• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:44 PM
Niliitwa kusaidia utekelezaji wa mauaji ya wakili nikielekea Gikomba – Mshtakiwa

Niliitwa kusaidia utekelezaji wa mauaji ya wakili nikielekea Gikomba – Mshtakiwa

Na RICHARD MUNGUTI

MSIRI wa polisi anayeshtakiwa pamoja na maafisa wanne wa polisi kwa mauaji ya kinyama ya wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wa teksi ameungama jinsi watatu hao walivyoangamizwa kisha wakatupa maiti zao katika mto miaka mitano iliyopita.

Bw Peter Ngugi alisimulia kwa kina jinsi alivyomwandama Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri kutoka mahakama ya Mavoko.

Bw Ngugi aliyetoa ushahidi akiwa upande wa mashahidi alisema baada ya Kimani na wenzake kutekwa nyara alipeleka gari la Muiruri hadi Limuru akalitupa kisha akarudi Mlolongo.

Usiku wa Juni 23/24, 2016 walienda kutupa miili ya watatu hao katika mto Athi River eneo la Donyo Sabuk.

Ngugi aliyejitetea mbele ya Jaji Jessie Lesiit alifichua kwamba mnamo Juni 23, 2016 aliagizwa na afisa wa polisi Wilson Kamau amwandame “mwizi fulani” katika mahakama ya Mavoko kisha amwarifu kisha amweleze kitakachoendelea.

“Kamau alinipigia simu nikielekea soko la Gikomba kununua mitumba na kuniagiza nifike katika kituo cha polisi cha Mlolongo kuna kazi anayotaka kunituma,” Ngugi alimweleza Jaji Lesiit.

Alisema alikuwa anatumiwa na Kamau kumpasha habari mbali mbali za uhalifu.

Ngugi alisema, “Niliacha kwenda Gikomba ambapo nilimpata Kamau na maafisa wengine wa polisi aliowataja kwa majina ‘Waingo’ na ‘Kamenchu’.”

Ngugi anashtakiwa pamoja na maafisa wa polisi Fredrick Leliman, Leonard Maina, Stephen Morogo na Sylvia Wanjohi.

Watano hao walikanusha kuwaua Kimani, Mwenda na Muiruri usiku wa Juni 23/24, 2016 katika eneo la Syokimau, Mlolongo, Athi River, Kaunti ya Machakos.

Kesi inaendelea.

You can share this post!

Uingereza na Wales katika makundi ya kifo droo ya Uefa...

Msiri wa polisi kwenye kesi ya mauaji ya Willie Kimani...

T L