• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mwakwere atawazwa kuwa msemaji wa Wadigo

Mwakwere atawazwa kuwa msemaji wa Wadigo

NA SIAGO CECE

MWANASIASA na balozi Chirau Ali Mwakwere sasa ndiye msemaji wa jamii ya Wadigo wanaopatikana katika maeneo ya Pwani.

Hii ni baada yake kutawazwa na wazee wa Kaya katika hafla ya kitamaduni katika uwanja wa Baraza Park, kaunti ndogo ya Matuga mnamo Jumamosi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na mamia ya wakazi na viongozi wengine kama vile Prof Hamadi Boga, Lung’anzi Chai, Khatib Mwashetani na wengineo.

Bw Mwakwere alivishwa mavazi ya kitamaduni yenye rangi nyekundu, nyeupe na nyeusi, na kwenye hafla hiyo, ngoma imechezwa na maombi maalum yakafanywa ili kumtawaza.

Akizungumza katika sherehe hiyo ya kufana, Bw Mwakwere alisema kutawazwa kwake si mchakato wa kisiasa, lakini ni njia moja ya kuwasilisha maswala ya jamii katika serikali ya kaunti na serikali kuu.

Baadhi ya wanajamii wakirindima ngoma za kitamaduni walimwonyesha upendo na kuitikia kutawazwa kwake.

“Timu yangu ina wasomi na wazee wa Kaya. Hatuna malengo yoyote ya kisiasa. Haja yetu kuu ni kuhakikisha kuwa tumewasilisha maswala yetu ya kijamii kwa viongozi wengine na kujiendeleza,” Bw Mwakwere alisema akisisitiza kuwa jamii hiyo ilikuwa imeachwa nje katika serikali.

Pia, alisema kuwa kamati itatengenezwa wakati wa siasa utakapofika, kuamua ni nani atakayekuwa kiongozi.

Bw Mwakwere atahudumu pamoja na naibu wake Marere Wa Mwachai na Prof Hassan Mwakimako kama Katibu Mkuu. Walidai kuwa kupitia uwakilishi wao, masuala mbalimbali ya Jamii, siasa na maendeleo yataelezwa vizuri.

Jopo hilo linatarajiwa kuanza kazi ikiwemo mikutano yao wiki ijayo wakilenga kukutana na viongozi katika serikali kuu ili kujieleza.

Kwa upande wao wazee wa Kaya, ambao walimchagua Bw Mwakwere walisema kuwa jamii ya WaDigo imewekwa kando hasa kwa maendeleo na nafasi katika serikali, jambo ambalo linafaa kuangaziwa.

Pia walieleza kuwa uwakikishi huo utasaidia kutatua maswala na changamoto zinazokumba WaDigo kama vile unyanyasaji wa ardhi. Walieleza kuwa jamii ya Waduruma pia itatengeza jopo lao la uwakilishi.

Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ugavana, Bw Chai, alisema kuwa ataunga mkono Bw Mwakwere katika jukumu lake jipya la kuwa msemaji wa jamii.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, na madiwani kutoka Kaunti ya Mombasa pia alikuwa kati ya waliohudhuria.

Kwa upande wake mbunge wa Zamani wa Matuga Hassan Mwanyoha amewakosoa wanaopinga uteuzi wa balozi Mwakwere kuwa msemaji wa Wadigo akishikilia kwamba ni sahihi huku akiwahimiza viongozi wa jamii ya Waduruma ambayo ni kati ya jamii kubwa kaunti ya Kwale kuiga mfano huo kwani hatua hiyo itahakikisha jamii hizo zinatambulika katika ngazi zote za serikali.

Viongozi wa jamii nyingine zinazoishi Kwale kama vile Wakamba wa Kwale walisema kuwa watashirikiana kuhakikisha kuna maendeleo katika jamii.

Hafla hiyo ilifanyika huku viongozi waliochaguliwa serikalini Kwale wakikashifu tendo hilo, wakisema ni la kumdhalilisha Gavana Fatuma Achani.

Wakiongozwa na Waziri wa Madini Uchumi wa Baharini Salim Mvurya, walisema kuwa Gavana Achani ndiye kiongozi na msemaji wa wakazi wote wa jamii.

“Tuna msemaji mmoja pekee wa jamii ya Wakwale na ni Bi Achani. Hata Rais William Ruto ndiye msemaji wa Kenya. Wale wanaojichagua wakati huu wanafanya kinyume na jamii yetu. Tunaomba kila mtu amuunge mkono Bi Achani,” Bw Mvurya alisema.

Alikuwa akizungumza katika hafla nyingine ya kuwahamasisha wakazi wa Kwale kuhusu ugonjwa wa saratani katika hospitali ya Rufaa ya Msambweni ambapo viongozi hao walikita kambi Jumamosi.

Seneta wa Kwale Issa Boi, Mwakilishi wa Kike Fatuma Masito, Mbunge wa Msambweni Feisal ambao pia walihudhuria walikashifu kutawazwa kwa Bw Mwakwere wakisema kuwa hio ni njia moja ya kutenganisha wakazi kikabila.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Kwale Chirema Kombo alisema ni hatia kwa makundi kujijumuisha na kufanya vitendo kikabila.

Bi Achani pia aliungwa mkono na madiwani wake wakisema kuwa wataendelea kufanya kazi naye licha ya tofauti za kisiasa.

Baadhi ya viongozi katika eneo la Pwani, tayari wameanza kujitayarisha kisiasa kabla ya mwaka wa 2027.

Wengi wakionyesha dalili ya kuhama kutoka vyama vyao na kujiunga na Bi Achani.

  • Tags

You can share this post!

Mke ajuta kutema ‘peremende’ kwa...

Songombingo Marereni walimu wa bodi wakiandamana kudai...

T L