• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 4:33 PM
Songombingo Marereni walimu wa bodi wakiandamana kudai malipo

Songombingo Marereni walimu wa bodi wakiandamana kudai malipo

NA ALEX KALAMA

HUKU mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) ukibisha hodi, shughuli za kawaida katika Shule ya Upili ya Marereni zimesambaratika baada ya walimu takribani 17 kuandamana wakidai malipo yao.

Walimu hao waliojawa na ghadhabu waliingia shuleni humo wakiwa na mabango baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kudaiwa kukataa kuwalipa.

Walimu hao waliandikwa na bodi ya shule hiyo.

Juhudi za mwalimu mkuu kukwepa shinikizo za walimu hao ziligonga mwamba kwani walimu hao walifunga lango kuu la shule hiyo na kulazimisha mwalimu huyo mkuu kusalia ofisini usiku kucha.

Kulingana na Bw Mwasambu Pole ambaye ni mmoja wa walimu shuleni humo, hatua hiyo imetokea baada ya kufunga shule mnamo Ijumaa.

Lakini inadaiwa kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo aliwaambia kuwa watapokea malipo yao mwezi Januari 2024.

“Tumeshangazwa na taarifa ya mwalimu mkuu wa shule hii baada ya kusema ya kwamba sisi walimu tulioajiriwa na bodi ya shule hatutapokea malipo yetu ya miezi mitatu hadi Januari 2024,” akasema Bw Pole.

Mwalimu huyo alisema waliahidiwa ujira wao wa mwezi Oktoba, Novemba na Desemba ungeingia mwakani.

“Ni hali ambayo imetuvunja moyo sana sisi na ndiyo maana tumeandamana na kukesha usiku kucha hapa shuleni tukidai haki yetu kwa sababu pia sisi tuna mahitaji na tuna familia zinatutegemea,” alisema Bw Pole.

  • Tags

You can share this post!

Mwakwere atawazwa kuwa msemaji wa Wadigo

Mama, 75, ashinda kesi ya kufurusha wanawe wa kiume...

T L