• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mwanamume apatikana amefariki gesti

Mwanamume apatikana amefariki gesti

Na SAMMY KIMATU

MWANAMUME mmoja alipatikana amefariki katika chumba cha kupanga kwenye mtaa mmoja wa mabanda kaunti ya Nairobi katika hali ya kutatanisha.

Akithibitisha kisa hiki, mkuu wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema kisa hiki kilitokea katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Reli katika wadi ya Landi Mawe.

Bw Odingo aliongeza kwamba marehemu alifika katika Dreamland Guest House na kukodi chumba cha kulala.

“Mwanamume huyo alikodisha chumba alale kama mteja yeyote yule wa kawaida. Hata hivyo, alipatikana keshoye akiwa amefariki mwili ukiwa kitandani,” Bw Odingo alisema.

Mwili wa marehemu ulitambuliwa kuwa wa Bw Benard Mwendwa Musyoka, 30, maarufu ‘Boy’ au ‘Swaleh’.

Marehemu alikuwa mhudumu wa matatu za Indimanje Sacco zinazohudumu katika maeneo ya Hillock na sokoni Muthurwa.

Hata hivyo, familia ya marehemu inasema kifo cha mwana wao kina hila na inataka polisi wachunguze zaidi.

Kwa mujibu wa mhudumu katika gesti hiyo ya Dreamland Bw Joel Mustapha, marehemu huwa ni mteja wa kila siku na hulala kati ya saa sita na saa saba za usiku.

Bw Mustapha aliambia Taifa Leo, kuwa mteja wake alifika mwendo wa saa tatu usiku akilalamika ‘asikii vizuri.’

Bw Mustapha alisema kwamba hulipisha Sh150 kwa kila chumba cha kulala.

“Alinomba maji anywe dawa na kuniomba nimletee jaketi avae. Mimi namjua kama mtu ambaye hupatwa na kifafa na wakati mwingine huwa na matatizo ya kupumua,” Bw Mustapha akaambia Taifa Leo.

Bali na hayo, Bw Mustapha alieleza kwamba marehemu alilala chumbani mwake na mteja mwingine kwa jina ‘Mwala’ anayeuza parachichi mtaani wa mabanda wa Kayaba.

“Mwala alirauka asubuhi na kumwacha marehemu akiwa amelala. Hakusema ikiwa alikuwa amefariki au la wakati wa kutoka,” Bw Mustapha akaeleza.

Kando na hayo, dadake marehemu, Bi Beatrice Mwikali Musyoka, 30, kifungua mimba katika familia ya watoto tisa, anayefanya kibarua na NMS mtaani Mukuru-Kwa Reuben alipinga ripoti ya kifo cha kakaye.

“Mwili wa kakangu ulikuwa na majeraha bafuni na kifuani huku akiwa na damu mdomoni mwake. Tunataka polisi wachunguze kisa hiki,” Bi Mwikali akaambia Taifa Leo.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Meritus Wanjala, alisema tukio hilo ni la tatu kufanyika katika vyumba vya kulala.

Gesti ya Dreamland. Picha/ Sammy Kimatu

Watu wawili walifariki mwaka 2020 wakiwa katika vyumba mbalimbali.

“Mwanamume mmoja aliteketea wakati wa moto ndani ya chumba baada ya kusahau kuzima mshumaa. Mwanamume mwingine alishambuliwa kwa kudungwa visu na watu wasiojulikana nje ya chumba chake cha kulala hapa mtaani,” Bw Wanjala akasema.

Kinara wa polisi kitengo cha upelelezi wa jinai kaunti ndogo ya Makadara Stephen Mutua, alisema wanachukulia tukio hilo kama kifo cha mtu aliyepatikana amefariki akiwa katika chumba cha kupanga.

Bw Mutua aliongeza kwamba ikiwa familia ya marehemu inataka uchunguzi kufanywa ili kubainisha kilichoua mtoto wao, basi waende kwake ofisini kufungua faili.

“Ikiwa familia ya marehemu inatilia shaka kifo cha mtoto wao, basi waje kwangu ofisini ili wafungue faili ili maafisa wa upelelezi wafanye uchunguzi wao na upasuaji wa mwili ukifanyika, ukweli utapatikana bila shaka,” Bw Mutua akanena.

You can share this post!

Juventus yapepetwa na Empoli nyumbani siku chache baada ya...

Clarke Oduor asuka pasi kusaidia Barnsley kuokota alama...