• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Juventus yapepetwa na Empoli nyumbani siku chache baada ya Ronaldo kujiengua kambini mwao

Juventus yapepetwa na Empoli nyumbani siku chache baada ya Ronaldo kujiengua kambini mwao

Na MASHIRIKA

JUVENTUS walipokezwa kichapo cha 1-0 na Empoli mnamo Jumamosi usiku katika mchuano wa kwanza wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) waliousakata bila nyota Cristiano Ronaldo ambaye amejiunga upya na Manchester United ya Uingereza.

Matokeo hayo yanasaza miamba hao wa soka ya Italia bila ushindi wowote kutokana na mechi mbili za ufunguzi wa msimu huu wa 2021-22. Kufikia sasa, Juventus ya kocha Massimiliano Allegri inashikilia nafasi ya 13 jedwalini kwa alama moja sawa na Cagliari na Spezia.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Empoli lilifumwa wavuni na Leonardo Mancuso katika dakika ya 21. Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Empoli kuwahi kusajili dhidi ya Juventus ambao ni mabingwa mara 36 wa taji la Serie A.

Mnamo 2020-21, Juventus waliokuwa wakinolewa na kocha Andrea Pirlo walikamilisha kampeni zao za Serie A katika nafasi ya nne jedwalini. Walianza msimu huu kwa sare ya 2-2 dhidi ya Udinese. Ronaldo ambaye ni raia wa Ureno na mchezaji wa zamani wa Real Madrid, aliachwa nje ya kikosi cha kwanza kilichotegemewa na Juventus katika mchuano huo.

Wakicheza dhidi ya Empoli mnamo Jumamosi, Juventus walisalia butu katika safu ya mbele huku wakionekana kulemewa katika takriban kila idara. Walitatiza ulinzi wa Empoli mara chache zaidi huku Manuel Locatelli akipoteza nafasi ya wazi ya kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mancuso, 29, ambaye alihudumu kambini mwa Juventus kwa miezi 18 bila ya kuchezeshwa katika kikosi cha kwanza alipata fursa ya kuwajibishwa dhidi ya Empoli japo akapoteza nafasi ya kufunga bao katika dakika ya 21.

Ushindi wa Empoli ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya Juventus katika kivumbi cha Serie A tangu 1999.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lewandowski afungia Bayern Munich mabao matatu na kuvunja...

Mwanamume apatikana amefariki gesti