• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 2:24 PM
Mwanamuziki maarufu wa injili ajikwaa na kuzama tena ulevini, alazwa hospitalini

Mwanamuziki maarufu wa injili ajikwaa na kuzama tena ulevini, alazwa hospitalini

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI maarufu wa nyimbo za injili kutoka eneo la Kati, Bw Dennis Mutara, amelazwa hospitalini, duru zikieleza amezongwa tena na uraibu wa pombe.

Bw Mutara alilazwa katika hospitali moja Kaunti ya Murang’a, Jumatatu mchana Septemba 11, 2023, na Wasamaria Wema waliofika nyumbani kwake katika eneo la Maragua.

Ijapokuwa watu walio karibu naye hawakueleza sababu halisi iliyomfanya kulazwa hospitalini, Taifa Dijitali ilithibitisha kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amezama tena kwenye uraibu wa matumizi ya vileo.

“Tunataka kumpa nafasi (Dennis) kupona. Tunampeleka hospitalini kwanza na baadaye katika kituo cha kurekebishia tabia (rehab). Anaonekana kuzidiwa na matumizi ya vileo,” akasema mmoja wa watu walio karibu na mwanamuziki huyo.

Kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao na mwanamuziki Karangu Muraya, Bw Mutara anasikika akiwazuia watu hao kumpeleka hospitalini, huku akisisitiza hakuwa mlevi.

“Niachilieni! Niachilieni….mimi sijakunywa pombe,” anasikika akisema.

Hii si mara ya kwanza Bw Mutara kuzama kwenye tatizo la ulevi na watu kujitokeza kumsaidia.

Mnamo Machi 2021, wasanii tofauti kutoka eneo la Kati walifanya mchango kumsaidia Bw Mutara kujisimamia tena, baada ya kuzidiwa na matumizi ya vileo.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari, Bw Mutara alikiri  alijipata kwenye matumizi ya vileo kutokana na ajali mbaya barabarani aliyopata, ambapo nusura apoteze maisha yake.

“Mimi sijui jinsi nilijipata kwenye tatizo hili. Nadhani hili linatokana na ajali niliyopata. Naomba Mungu aninusuru,” akasema Bw Mutara.

Kwenye mchango huo, wanamuziki na mashabiki wake walimsaidia kununua gari jipya, lililokuwa limepangiwa kumsaidia kwenye usafiri kwenda shoo au kwenda hospitalini.

Kutokana na matukio ya Jumatatu, viongozi kadhaa walijitokeza na kusema kuwa kando na maombi, mwanamuziki huyo anahitaji matibabu maalum.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri alisema amezungumza na mwenzake wa Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, kubuni njia watakayomsaidia mwanamuziki huyo.

“Nimezungumza na mwenzangu Irungu Kang’ata kuhusu vile tutashirikiana kumnusuru ndugu yetu Dennis,” akasema.

Mwanamuziki huyo anasifika kwa vibao vingi maarufu kama vile “Tigana na Andu” (Achana na Watu), “My Lover” (Mpenzi Wangu), “Turi a Ngai” (Sisi ni wa Mungu) kati ya vingine.

  • Tags

You can share this post!

Wakimbizi wanavyofaulu kuvuna donge jijini licha ya...

Kiongozi wa Upinzani Tanzania Tundu Lissu ashukuru polisi...

T L