• Nairobi
  • Last Updated December 3rd, 2023 8:00 PM
Wakimbizi wanavyofaulu kuvuna donge jijini licha ya changamoto ya uraia

Wakimbizi wanavyofaulu kuvuna donge jijini licha ya changamoto ya uraia

NA LABAAN SHABAAN

Annociate Dusabe, 27, ni mmoja wa wakimbizi zaidi ya 80, 000 wanaosaka tonge na makao jijini Nairobi na safari yake ya miaka sita imekumbwa na pandashuka si haba.

Hatua zake za maisha zinaakisi hali halisi ya wakimbizi wenzake wa mijini wanaozongwa na vizingiti vya kupata vibali vya biashara, huduma za afya na makao.

Katika kipindi cha kuishi Kenya, Dusabe amekuwa mchuuzi wa mitumba jijini hasaa eneo la Kabiria, Kawangware.

“Nimepitia changamoto nyingi kuchuuza mitumba barabarani, kuchomwa na jua kali, uchovu na ukosefu wa vibanda vya biashara na sasa imebidi nitafute mbinu nyingine ya kutega uchumi,” Dusabe anaambia Akilimali.

Kadhalika, amewahi pia kuwa msusi aliyeajiriwa katika saluni ila sasa anajikakamua kuwa mshonaji mavazi na anaamini kazi hii itakuwa na pato kwa sababu ameanza kupata hela akiwa mwanagenzi.

Miezi sita iliyopita Dusabe alijisajili katika mpango wa mafunzo ya ushonaji mavazi na mabegi ya vitenge na vitambaa vya jeans.

“Nimetaka kufungua duka langu kwa muda mrefu na huu ndio wakati mwafaka kwa sababu mashirika yamejitolea kuinua maisha ya wakimbizi,” anaeleza Dusabe.

“Ninafurahia sasa kuwa nimeanza kupata pesa nikiendelea kusomea ushonaji na angalau huhudumia wateja watatu kwa wiki nikiuza begi kati ya Sh500 na Sh2, 000,” anaongeza.

Shirika lisilo la kibiashara la kushughulikia maslahi ya wakimbizi la Umoja Refugee Camp (URC) kupitia tawi tanzu la Umoja Refugee Creative linaendeleza mpango wa mafunzo bila malipo kusaidia makundi ya wakimbizi kuafikia uwezo wa kiuchumi na kujitegemea.

“Tunapigwa jeki na mashirika kama Refuge Point na Cohere kuinua wakimbizi na wahamiaji ili wakabili changamoto wanazopitia kutafuta maisha katika nchi zingine,” anaeleza Jonas Ndayisenga, Mkurugenzi mtendaji na mwanzilishi mwenza wa URC.

Ndayisenga anaendelea kueleza kuwa URC inajumuisha shughuli za ujasiriamali kupitia mashirika ya mikopo na akiba mijini (USLA) ambapo mafunzo hutolewa pamoja na fedha za kuwezesha mipango.

Vile vile waliopokea mafunzo husaidiwa kuanza safari ya kujitegemea na hufuatiliwa ili wasilemewe na changamoto za biashara ndogo ndogo na za kadri ambazo aghalabu hulemea wajasiriamali wakafunga biashara zao.

Miongoni mwa matatizo wanayokabiliwa nayo wakimbizi wanabiashara ni ukosefu wa stakabadhi za utambuzi zinazowezesha utoaji wa leseni na vibali vya biashara na upatikanaji wake ni adimu sana.

“Mchakato wa kupata vitambulisho vya Kenya unaenda pole pole sana kwa hivyo unachelewesha upatikanaji wa vibali vya biashara na nambari za ulipaji ushuru (KRA PIN),” Dusabe anakiri.

Mmoja wa wakimbizi walionufaika na mpango wa inua dada aonyesha sabuni ya maji wanayotengeneza na kuuza. PICHA | LABAAN SHABAAN

Naye Ndayisenga anasema mashirika ya wakimbizi yanafanya kazi na washikadau serikalini na mashirika ya kimataifa kuimarisha na kurahisha mchakato wa kushughulikia stakabadhi muhimu kwa wakimbizi wajiendeleze kibiashara na wakubaliwe nchini.

URC inaripoti kuwa 90% ya walionufaika na mpango wa mafunzo ya stadi za kibiashara  wameanza kusimamia biashara zao baada ya kuidhinishwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Baadhi ya bidhaa zinazouzwa na wakimbizi ni sabuni ya maji, mavazi aina mbalimbali, vibeti na mabegi nyinyi yazo zikitengenezwa nao wenyewe.

Maendeleo haya yamewashushia mizigo wakimbizi wanabiashara ambao awali walikuwa wanakamatwa na askari wa kaunti na vibanda vyao vya biashara kuharibiwa.

  • Tags

You can share this post!

Owalo awataka wabunge kubadilisha sheria na sera za sekta...

Mwanamuziki maarufu wa injili ajikwaa na kuzama tena...

T L