• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mwangaza aanza kukwaruzana na madiwani tena

Mwangaza aanza kukwaruzana na madiwani tena

GITONGA MARETE NA DAVID MUCHUI

GAVANA wa Meru, Kawira Mwangaza, ameanzisha vita na madiwani baada ya kukaidi bunge la kaunti na kuzindua miradi ya Hazina ya Mitambo na Uchukuzi (MTF).

MTF iko katika wizara ya Uchukuzi na Miundombinu chini ya idara ya Barabara na imeingia katika makubaliano na serikali za kaunti kuhusu usambazaji, ujenzi na ukarabati wa barabara.

Bi Mwangaza alisema uongozi wake utalipa Sh531 milioni kwa MTF ambazo zitatumika katika miradi ya uboreshaji wa barabara iliyopewa jina “Mwangaza Barabarani”.

Alisema utawala wake hautaruhusu wanakandarasi wa ndani kutengeneza barabara, akiwatuhumu kufanya kazi mbovu na kujihusisha na ufisadi.

“Mwaka wa fedha uliopita tulilipa wanakandarasi Sh225 milioni na walifanya kilomita 295 huku MTF ilifungua zaidi ya kilomita 200 kwa kutumia Sh90 milioni. Ni wazi, kwamba MTF inatumia pesa kidogo kufanya kazi bora,” Bi Mwangaza alisema.

Gavana huyo alisema Sh195 milioni zitatumika kuweka lami barabarani huku Sh336 milioni zitatumika kufungua barabara mpya na kuweka daraja zilizopo ambazo kazi zake zitaanza Januari 2024.

“Barabara zetu zimeharibiwa na El Nino na tunataka kuhakikisha kuwa zimekarabatiwa kufikia Juni mwaka ujao na tuna imani na MTF kuwa itafanya kazi bora,” akaongeza Bi Mwanagaza.

Wiki iliyopita, wawakilishi wa wadi walipitisha hoja ya kumtaka gavana kukata uhusiano na MTF na kutoa zabuni za ujenzi wa barabara kwa wanakandarasi wa ndani. Lakini gavana huyo alisema wanakandarasi wanafanya kazi duni na ni wafisadi.

Walidai kuwa hatua ya gavana huyo ya kushirikiana na MTF ni njia mojawapo ya kupoteza mabilioni ya fedha za walipa ushuru.

“Tuna ushahidi kwamba pesa zinaingia kwenye mifuko ya watu ambao wanashirikiana na maafisa wa MTF. Gavana sasa yuko peke yake na tunasubiri kuona jinsi taasisi isiyo na uwezo wa kutosha itajenga barabara zetu,” alisema MCA wa Abogeta Magharibi, Dennis Kiogora.

Wakizungumza Jumatano kwenye bunge la kaunti baada ya kuzindua mradi huo, madiwani walisema kwa kuwa gavana huyo amekaidi ushauri wao, watawasiliana na wakazi na kuwaeleza yaliyotokea.

  • Tags

You can share this post!

Vibanda vinavyofuga wahuni na wahalifu Ruiru 

Kwani tutawafunza kila kitu? Arsenal, Man City waokolea...

T L