• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Mwathi achaguliwa mwenyekiti wa kamati ya usalama bungeni

Mwathi achaguliwa mwenyekiti wa kamati ya usalama bungeni

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Limuru Peter Mwathi amechaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama kuchukua mahala pa marehemu Paul Koinange.

Marehemu Koinange ambaye alihudumu kama Mbunge wa Kiambaa alifariki mnamo Machi 31, 2021, baada ya kuugua mwa muda mfupi.

Hadi Jumanne alipochaguliwa na wanachama wa hiyo kamati ya Usalama Bw Mwathi alikuwa akihudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Leba na Masuala ya Kijamii.

Kando na hayo yeye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Hadhi na Mamlaka ya Wabunge.

Naibu mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Usalama Bi Fatuma Gedi ambaye awali alikuwa ameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo alijiondoa kinyang’anyironi dakika za mwisho.

Bi Gedi, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Wajir, alisema kuwa alijiondoa baada ya kushauriwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Waziri Mkuu wa zamani aliniambia nimpishe mwenzetu Bw Peter Mwathi kwa sababu alionyesha imani naye,” akawaambia wanahabari baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo ulioendeshwa katika ukumbi mkuu wa mijadala, Bunge la Kitaifa.

Kwa upande wake Bw Mwathi aliwashukuru wanachama wa Kamati hiyo ya Usalama kwa kuonyesha imani naye na kumpa nafasi ya kuwa mwenyekiti wao.

“Naahidi kwamba tutafanyakazi pamoja kwa ushirikiano. Marehemu Koinange alikuwa rafiki wangu mkubwa na nitafuata nyayo zake. Hata hivyo, ningependa kuungama kuwa viatu vilivyoachwa na Koinange ni kubwa mno lakini nitajaribu kuvivaa,” mbunge huyo wa Limuru akaeleza.

Bw Mwathi aliahidi kutekeleza kazi zote za kamati hiyo ambazo marehemu Koinange alikuwa akishughuli nazi kama mpango wa kuleta amani katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya.

You can share this post!

Maabara ya kupima Covid-19 kwenye uwanja wa ndege wa...

Trump azindua blogu ya kuchapisha taarifa muhimu kutoka...