• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Mzozo wa shamba wamtia Mwanawe Meja Jenerali Mstaafu Joseph Ndolo taabani

Mzozo wa shamba wamtia Mwanawe Meja Jenerali Mstaafu Joseph Ndolo taabani

Na RICHARD MUNGUTI

MZOZO wa muda mrefu wa shamba la ekari 3,000 kati ya familia ya aliyekuwa Meja Generali Joseph Musyimi Ndolo na wakazi 84 wa Kalimbini (B) umemsukuma na kupelekea mwanawe mkuu huyo wa majeshi kushtakiwa.

Andrew Ndola Ndolo anakabiliwa na mashtaka ya wizi wa mabavu ambao adhabu yake ni kunyongwa akipatikana na hatia.

Ndola aliyeshtakiwa Julai 2022 katika Mahakama ya Kilungu, Kaunti ya Makueni alifika kortini Mei 2, 2023 lakini kesi haikuendelea.

Mawakili wa Ndola walimweleza hakimu mkazi Bw Godfrey Okwengu upande wa mashtaka haujamkabidhi na nakala zote za mashahidi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma amemshtaki Ndola kwa kuvamia mashamba ya familia 84 miezi 10 iliyopita.

Ndola ambaye ni mfanyabiashara maarufu Nairobi anakondolewa macho na vifungo virefu endapo upande wa mashtaka utathibitisha kesi dhidi yake.

Miongoni mwa mashtaka 12 dhidi ya Ndola ni wizi wa mabavu , ubomoaji nyumba, kuaribu mali , kuteketeza tingatinga ya thamani ya Sh5milioni, kupiga watu na kuwajeruhi, kuvunja nyumba na kuiba, kuharibu mali ya mamilioni ya pesa na kuvuruga amani.

Ndola anadaiwa alitekeleza uhalifu huo mnamo Julai 2 na 21 mwaka uliopita.

Alikanusha mashtaka yote aliposhtakiwa mbele ya Bw Okwengu mnamo Machi 20, 2022.

Hakimu aliorodhesha kesi hiyo kuanza kusikizwa Mei 2, 2023.

Shtaka la kwanza dhidi ya Ndola lasema mnamo Julai 21, 2022 katika kijiji cha Kalimbini (B) lokesheni ndogo ya Kalimbi kaunti ya Makueni akiwa amejihami kwa silaha pamoja na watu wengine alimwibia Titus Ngile Masila nguo, viatu, mashine ya kuosha nywele,televisheni ya inchi 43, simu muundo wa Samsung na Huawei zote za thamani ya Sh195,000.

Shtaka hilo linasema wakati wa wizi huo walimshambulia Titus Ngile Masila.

Ushahidi uliowasilishwa kortini ni pamoja na picha za nyumba zilizoteketezwa, tingatinga na bidhaa za nyumbani.

Kulingana na ushahidi Ndola alikuwa ameandamana na wahuni wakati wa mashambulizi hayo ya Julai 1 na 21 mtawalia.

Hawakuwa na kibali cha mahakama kikiruhusu walalamishi kutimuliwa.

Ndola ameshtakiwa kuharibu makazi yaliyostawishwa ya gharama ya Sh1, 140, 000 na Sh 2,710,000 ya Bw Ngile na jirani yake Bw Chris Nzomo Ngila.

Ndola pia amekana shtaka la kuchoma tinga tinga la thamani ya Sh5, 003,000 ya kampuni ya Azicon Kenya Limited.

Pia alishtakiwa kumpiga na kumjeruhi dereva wa tinga tinga hilo Benedictor Mwangangi Muse kwa madai alikataa kutekeleza amri ya Ndola.

Pia ameshtakiwa kuwajeruhi Kennedy Mutua Kamuya, Joseph Munganya Masika na Timothy Musyoka Maitha.

Tangu Meja Jenerali Ndolo afariki kwenye barabara 1984 mzozo mkali ulizuka kuhusu shamba lake la ekari 9,000 karibu na mji wa Sultan Hamud kwenye barabara ya Mombasa-Nairobi.

Wakazi hao wa Kalimbini (B) waliwasilisha kesi dhidi ya familia ya Ndolo.

Miongoni mwa walioshtaki familia ya Meja Generali Ndolo ni pamoja na Rais wa Mahakama ya Rufaa Daniel Musinga na wakili mwenye tajriba ya juu Muema Kitulu na aliyekuwa afisa mkuu serikalini Mwelu Gatuguta.

Walalamishi wanaomba mahakama kuu iamuru wapewe nakala za umiliki wa mashamba waliyouzwa na marehemu Josiah Kaumbulu.

Mashahidi saba wameorodheshwa kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Ndola.

Kesi hiyo iliahirishwa Julai 4, 2023.

Akiahirisha kesi hiyo Bw Okwengu alisema: “Upande wa mashtaka haujamkabili mshtakiwa na nakala zote za mashahidi. Itabidi hii kesi iahirishwe. Naamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala zote za mashahidi.Kesi itaanza kusikizwa Julai 4, 2023.”

 

 

  • Tags

You can share this post!

Muuzaji nyama taabani kwa kuiba pesa za mauzo

Wakili aachiliwa kwa dhamana katika kesi ya ulaghai wa hisa

T L