• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
Namna rahisi ya kuandaa Pizza

Namna rahisi ya kuandaa Pizza

Na MARY WANGARI

IWAPO kuna mlo ambao huwafurahisha mno watoto na watu wazima kwa jumla basi ni pizza, chakula ambacho asili yake ni Italia.

Wengi wanaposikia jina pizza, wazo la kwanza linalowajia ni kwamba ni chakula cha wakwasi wanaojiweza kifedha.

Huenda ni kweli ikizingatiwa kwamba pizza aghalabu huuzwa kwa bei ghali ambayo wengi hawawezi kuimudu.

Lakini nani alisema huwezi kujiandalia pizza hapo hapo nyumbani kwa kutumia vifaa na viungo vinavyopatikana kirahisi?

Hii leo, tutajifunza jinsi ya kuandaa pizza kwa ustadi na kwa njia rahisi.

Vinavyohitajika

  • ½ pakiti unga wa ngano
  • Mafuta ya kupikia
  • ¾ nyama ya kuku
  • ½ mtindi
  • 1 kitunguu maji kikubwa
  • 1 kijiko kidogo cha hamira
  • ½ kijiko cha chumvi (kiasi cha haja)
  • 2 mayai
  • 1 kidonge cha jibini (cheese)
  • 1 kijiko bizari ya kuku, tandoori,
  • Pilipili
  • Kitunguu saumu
  • Mtindi
  • 2 karoti kubwa
  • 1 kijiko tomato paste, au ketchup ukipenda

Maandalizi

Katika karai safi, loweka hamira na chumvi kwenye maziwa ya vuguvugu (unaweza ukatumia maji ya vuguvugu pia) na kisha uiache kidogo ili iyeyuke vyema.

Usitie hamira na chumvi nyingi kwa sababu pizza haifai kufutuka.

Ongeza ngano, custard na uikande vyema, hakikisha maziwa au maji yanazidi kiasi kuliko unga ili donge lako liwe laini.

Subiri kwa dakika 15 ili donge lako liumuke kisha ulisukume kwa kutumia kifaa cha kupikia chapati liwe na ukubwa wa wastan.

Katakata kuku vipande vidogo vidogo na kisha uvisafishe. (Unaweza pia ukatumia nyama ya ng’ombe iliyosagwa)

Katika sufuria safi, katakata kitunguu maji, mimina mafuta ya kupikia na kisha ubandike jikoni.

Mafuta yakishashika moto tia kitunguu maji na usubiri vigeuke rangi, tia vipande vya kuku, miminia chumvi huku ukikoroga vyema.

Safisha na ukate vipande pilipili mboga, nyanya na karoti kisha uvitie kwenye kuku huku ukizidi kukoroga.

Ongeza viungo vingine ikwemo bizari ya kuku, tandoori, asali, nyanya na mtindi huku ukikoroga rojo lako linalozidi kuwa zito.

Kwa kutumia umma toboa mashimo kwenye donge lako kisha upake tomato paste upande wa juu.

Kwa kutoboa donge lako la unga unawezesha moto kupita kirahisi na kuruhusu pizza ipate hewa.

Ongeza rojo lako la kuku tia jibini ya kutosha na ikiwa huna au hupendi jibini, unaweza ukamiminia mayai uliotwanga.

Tia kwenye oveni tayari kwa kuoka kwa dakika 30 tu.

Pizza yako ipo tayari kuliwa na uweza ukajiburudisha kwa sharubati baridi.

Ikiwia huna oveni usiwe na shaka. Jaza jiko lako makaa na ulipepete hadi litakapowaka.

Chukua sufuria safi uipake siagi na kisha utandaze vyema unga wa ngano uliosalia kabla ya kutia mchanganyiko wako.

Katika sufuria nyingine kubwa zaidi ijaze mchanga na uibandike kwenye jiko hadi lipate moto.

Chukua sufuria yenye pizza uitie ndani ya sufuria lenye mchanga kisha ufunike na kusubiri kwa dakika 30. Pizza yako itakuwa tayari kwa kuliwa.

You can share this post!

Maafisa wa polisi wako katika mazingira duni, yaboreshwe...

Kilio cha wafugaji wa kuku Kiambu