• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Kilio cha wafugaji wa kuku Kiambu

Kilio cha wafugaji wa kuku Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

WAFUGAJI wengi wa kuku Kaunti ya Kiambu wanapata hasara, chanzo kikiwa ni kudorora kwa bei ya mayai.

Wafugaji hao wanasema hali hii inatokana na mayai yanayoingizwa nchini kutoka kwa mataifa jirani.

Wafugaji wa hapa wamelazimika kuuza mayai kwa bei ya chini.

Bi Salome Wairimu kutoka kijiji cha Ngoingwa, Thika, anasema bei ya chakula cha kuku ni ya juu mno, hali inayofanya wafugaji washindwe kuendelea na biashara zao kama awali.

Meneja mkuu wa chama cha ushirika cha wafugaji hao Bw John Njenga anasema vifaa vya matumizi katika sekta hiyo ni vya bei ya juu sawa na chakula cha kuku ambacho ni cha bei ya juu.

Anazidi kueleza kuwa vyama vingi vya ushirika vimevunjika kutokana na hali ngumu ya kuendesha biashara ya ufugaji.

“Biashara hiyo haina faida tena kama ilivyokuwa hapo awali, hali inayofanya wafugaji hao kufanya biashara tofauti kama kilimo cha parachichi na macadamia,” alifafanua Bw Njenga.

Hata hivyo meneja huyo ameitaka serikali kuingilia kati ili kuwaokoa wafugaji hao.

Wakulima wanaiomba serikali kuweka bei ya mayai kuwa sawa na kupunguza malipo ya ushuru.

Gunia moja la chakula cha kuku linauzwa Sh3,000 kutoka kwa bei ya zamani ya Sh2,500.

Bw Njenga alisema wafugaji wengine wamekosa kazi huku maisha yakiwalemea.

Bw Zacharia Munyambu ambaye ameendesha biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 20 anasema amefunga shughuli zake zote.

“Mimi kama mfugaji wa kuku kwa muda huo wote nimeshindwa la kufanya wakati nina watoto walio shuleni na mahitaji yakiwa ni mengi,” alifafanua Bw Munyambu.

Bi Anne Wanjiku anasema tayari biashara yake imeshuka kabisa huku wateja wake wengi wakisitisha kununua mayai kutoka kwake.

“Tunaiomba serikali kuingilia kati kuona ya kwamba nchi jirani zinadhibitiwa kuzima hali ya ‘kuingiza mayai kwa wingi hapa nchini’,” akasema Bi Wanjiku.

You can share this post!

Namna rahisi ya kuandaa Pizza

Shikanda asema ladha ya ligi iliisha Juni 30