• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Ndoa baina ya makanisa na Rais Ruto yaanza kuisha ladha

Ndoa baina ya makanisa na Rais Ruto yaanza kuisha ladha

WANDERI KAMAU NA VITALIS KIMUTAI

UHUSIANO uliokuwepo baina ya viongozi wa kidini nchini na vigogo wakuu wa muungano wa Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi mkuu uliopita na punde baada ya kuingia mamlakani mwaka jana unaonekana kuyumba, baadhi yao sasa wakikosoa serikali vikali.

Kauli za viongozi hao wakiwemo maaskofu wa hadhi zinaonyesha ‘ukuruba wa kiroho’ kati yao na wanasiasa wakuu serikalini umeingia doa.

Uhusiano huo uliingia doa zaidi Jumapili baada ya Kiongozi wa Wengi katika Bunge, Kimani Ichung’wa na mwenzake wa Seneti Aaron Cheruiyot kuwafokea maaskofu Jackson Ole Sapit wa Kanisa la Kianglikana (ACK) na mwenzake Anthony Muheria wa Jimbo la Nyeri, Kanisa Katoliki.

Kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, vigogo wa Kenya Kwanza -wakiongozwa na Rais William Ruto- walikuwa marafiki wakubwa wa wakuu wa makanisa, wakiahidi kwamba wangedumisha uhusiano huo hata baada ya kushinda uchaguzi.

Katika hali inayoonekana kama hatua ya kutimiza ahadi yao, Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua waliwaalika viongozi hao kwa kikao maalum cha “kuitakasa Ikulu” siku chache baada ya kuapishwa kama rais na naibu rais.

Hata hivyo, urafiki huo umegonga mwamba baada ya wakuu hao wa kidini kuanza kuilaumu serikali kwa kupiga domo tu na kutotimiza ahadi ilizotoa.

Baadhi ya viongozi ambao wamejitokeza wazi kuukosoa uongozi wa Kenya Kwanza, ni Askofu Ole Sapit na Askofu Mkuu Muheria.
Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, Askofu Sapit aliwaongoza viongozi wa kanisa hilo kuilaumu serikali kutokana na gharama ya juu ya maisha na changamoto nyingine zinazoikumba nchi.

“Mtazamo wetu wa kweli kama Kanisa ni kwamba, kumekuwa na upigaji domo mwingi na utoaji visingizio kuliko juhudi za kweli kutatua changamoto zinazoikumba nchi. Tunairai serikali kutotoa ahadi tu, bali ikumbatie juhudi za kweli kutatua matatizo yanayowakumba Wakenya,” akasema Askofu Sapit kwenye kikao na wanahabari baada ya mkutano huo.

Askofu huyo pia alikosoa vikali kauli iliyotolewa na Bw Gachagua, akiifananisha serikali ya Rais Ruto na kampuni yenye hisa, ambapo wenye hisa nyingi ndio huwa wanapata faida.

“Tumeshuhudia mapendeleo ya kikabila katika uteuzi wa nyadhifa za umma serikalini. Wakenya wanafaa kupewa nafasi sawa bila kujali asili yao,” akasema askofu huyo.

Kinaya ni kuwa, Askofu Sapit alikuwa kati ya viongozi wa makanisa waliofika katika Ukumbi wa Bomas ‘kumsindikiza’ Dkt Ruto, alipotangazwa mshindi wa urais na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (IEBC), Bw Wafula Chebukati.

Mnamo Julai, Askofu Muheria alimkashifu vikali Rais Ruto, akimtaja kama “kiongozi asiyejali”.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Julai 15 mwaka huu, askofu huyo alisema serikali ya Rais Ruto inafaa kuonyesha uungwana na ubinadamu.

“Uongozi unafaa kuwa wenye ubinadamu, huruma na kujali. Kwa sasa, kiongozi aliyepo ni mwenye msimamo mkali, matusi, dharau na wa kulazimisha. Tunaelekea katika uongozi mbaya sana, na hii ndiyo sababu viongozi wa kidini wamejitokeza kuongea,” akasema askofu huyo.

Kiongozi huyo aliurai uongozi wa Kenya Kwanza kuzungumza na viongozi wa kidini, ili “kubuni utaratibu mzuri wa uongozi bila vitisho na ushindani usiofaa”.

Hata hivyo, viongozi wa Kenya Kwanza wamewakosoa maaskofu hao wawili, wakiwataja kuwa “maajenti wa mrengo wa Azimio la Umoja”.

Bw Kimani Ichung’wah, Jumapili, alikashifu msimamo wa maaskofu hao alipokuwa katika Kaunti ya Kericho.

“Askofu Muheria na Askofu Sapit walimuunga kiongozi wa Azimio, Raila Odinga wazi wazi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, na wameendelea kufanya hivyo hata baada ya uchaguzi. Hata wanapozungumza, tunajua wanazungumza kwa niaba ya nani,” akasema Bw Ichung’wa.

Bw Ichung’wa, ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu, alisema viongozi wa kidini wanafaa kuikosoa serikali kwa njia mwafaka, bila mapendeleo yoyote.

“Askofu Sapit hapaswi kufunga macho kuhusu athari mbaya za kiuchumi za vitendo vya watu aliowaunga ,” akaongeza.
Kwa upande wake, Seneta Aaron Cheruiyot alisema Wakenya wanafaa kuipa nafasi serikali ya Rais Ruto kutimiza ahadi ilizotoa bila “kukubali kupotoshwa”.

“Sote tunafaa kuunga mkono nia nzuri za serikali kuimarisha uchumi wetu ili kukoma kutegemea mikopo,” akasema.

Awali, Baraza la Makanisa Kenya (NCCK) pia lilikosoa serikali kwa kubebesha raia mzigo mzito wa ushuru na gharama ya maisha kupitia Sheria ya Fedha ya 2023 lakini wito wao ulipuuzwa huku Rais Ruto akiitetea vikali.

Mwenyekiti wa NCCK, Timothy Ndambuki alimwambia Dkt Ruto kuwa “ viongozi wa makanisa walihofia kutamauka kwa Wakenya kungetumbukiza nchi katika misukosuko n ahata ghasia.

Wito kama huo ulitolewa na Baraza la Maaskofu wa kanisa Katoliki chini ya mwenyekiti wao Askofu Kivuva Musonde lakini serikali iliupuuza.

Akihutubu Julai katika Kaunti ya Murang’a, Bw Gachagua alipuuza wito wa baadhi ya viongozi wa kidini kwa Rais Ruto kufanya mazungumzo na Bw Odinga kutokana na maandamano yaliyokuwa yakiendeshwa na Azimio la Umoja.

“Maaskofu, kwa hekima, mnapomwambia Rais Ruto kufanya mazungumzo na mnafiki (Bw Raila), mnamwambia akiuke Katiba. Ukweli ni kuwa (Raila) anatafuta handisheki, na hatutakubali,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mzozo wa uongozi unavyotikisa kanisa la Kianglikana...

Ni rasmi sasa kwamba Kenya itapeleka polisi 1,000 nchini...

T L