• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Ni rasmi sasa kwamba Kenya itapeleka polisi 1,000 nchini Haiti baada ya UNSC kutoa idhinisho

Ni rasmi sasa kwamba Kenya itapeleka polisi 1,000 nchini Haiti baada ya UNSC kutoa idhinisho

NA MASHIRIKA

SASA ni rasmi kwamba Kenya itaongoza Kikosi cha Walinda Usalama kutoka mataifa mbalimbali kuelekea nchini Haiti kupambana na magenge ya wahalifu ambayo yamevuruga amani katika taifa hilo la eneo la Caribbean.

Hii ni baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) Jumatano kutoa kibali cha kutumwa kwa ujumbe huo wa walinda usalama ambao wanatarajiwa kutoa ulinzi kwa miundomsingi muhimu kama vile viwanja vya ndege, bandari, shule, hospitali, majengo ya serikali na mizunguko muhimu ya barabarani.

Kikosi hicho cha MSSM pia kitapiga jeki operesheni za kiusalama zinazoendeshwa na Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) chenye jumla ya maafisa 10,000 na ambao walemewa na magenge hayo yenye silaha hatari.

Kenya imekubali kutuma angalau maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti na nchi nyingine pia zinatarajiwa kutoa rasilimali za kufanikisha kibarua hicho.

Karibu watu 3,000 waliuawa nchini Haiti kutoka Oktoba 2022 hadi Juni 2023, baada ya magenge kuteka sehemu kubwa ya nchi hiyo, haswa jiji kuu la Port-au-Prince, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Wakazi wengi wamehama makazi mbalimbali kutoroka magenge ya wahalifu ambayo yamekuwa yakitekeleza mauaji, utekaji nyara na uporaji mali.

Ripoti zinasema kuwa magenge hayo yanayodaiwa kudhaminiwa na vyama vya kisiasa yameendeleza udhibiti wao wa Haiti tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise.

Hakuna chaguzi zozote za ubunge au udiwani zimefanywa katika kipindi cha miaka mingi, hali inayochangia uwepo wa ombwe la uongozi.

Maafisa wanasema lengo moja la kikosi cha walinda usalama wa MSSM wanaoongozwa na Kenya ni kurejesha mazingira ya usalama ili kutoa nafasi kwa uchaguzi kufanywa.

Duru katika serikali ya Kenya zinasema kuwa Kenya itatuma wanajeshi wake nchini Haiti kufikia Januari 2024.

Jumla ya wanachama 13 wa baraza la UNSC walipiga kura ya kuunga uamuzi wa kutumwa kwa vikosi vya usalama nchini Haiti, huku Urusi na China zikisusia upigaji kura.

Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Haiti Jean Victor Geneus alitaja uamuzi huo kama “utakaoleta matumaini kwa watu wa nchi hiyo ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu.”

“Ama kwa hakika uamuzi huu unaonyesha kuwa mataifa ya ulimwengu yanaungana na watu wetu wanaohitaji usaidizi,” akasema Geneus.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken alisifu uamuzi huo wa UNSC.

“Tunapongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuidhinisha kutumwa kwa vikosi vya usalama kutoka mataifa mbalimbali nchini Haiti, hatua muhimu ya kutoa usaidizi ambao nchi hiyo imeomba ili kurejesha usalama. Tunashukuru Kenya na Ecuador kwa ushirikiano wao katika juhudi hizi,” akasema baada ya upigaji kura.

Hatua ya Urusi na China kususia upigaji kura ni ishara kwamba nchi hizo hazikuidhinisha uamuzi lakini hazingeweza kuuzuia.

TAFSIRI: CHARLES WASONGA 

  • Tags

You can share this post!

Ndoa baina ya makanisa na Rais Ruto yaanza kuisha ladha

Tineja mmoja kutoka Ganze auawa kwa kukatwa shingoni

T L