• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Ni kweli Mackenzie anataseka gerezani, tume ya haki yaambia mahakama

Ni kweli Mackenzie anataseka gerezani, tume ya haki yaambia mahakama

NA MKAMBURI MWAWASI

TUME ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNHCR) imekubaliana na mshukiwa mkuu wa vifo vya Shakahola, Bw Paul Mackenzie, kwamba haki zake nyingi zinakandamizwa akiwa kizuizini.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa mahakamani Shanzu na tume hiyo, imebainika malalamishi mengi ya Bw Mackenzie na washukiwa wengine tisa kuhusu hali mbaya wanayopitia gerezani ni kweli.

Ripoti iliyowasilishwa kortini na wakili wa KNHCR Faiza Musa, ilionyesha kuwa vitendo vya wasimamizi wa magereza, vilikuwa unyanyasaji na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wafungwa.

Iliongeza kwamba maafisa hao wa polisi walifanya hivyo kwa kukusudia badala ya kulinda haki za washukiwa na kuzingatia kanuni za haki za binadamu.

Tume hiyo iliiambia mahakama ya Shanzu, kaunti ya Mombasa kwamba Paul Mackenzie alidhulumiwa akiwa rumande katika gereza la Shimo la Tewa na kunyimwa haki zake za kimsingi.

“Kutokana na uchunguzi uliofanywa na tume hii, ilionekana kwamba kutokana na madai yaliyotolewa na washukiwa, inatosha kusema kwamba walidhulumiwa,” ilisoma ripoti.

Ripoti hiyo ilionyesha kwamba kuhusu tuhuma za ukiukaji wa uhuru na haki za kibinadamu dhidi ya wafungwa wanaoshikiliwa katika gereza la Shimo la Tewa, Kilifi na Malindi.

Kutokana na uchunguzi na matokeo, ripoti hiyo ilionyesha kwamba Mackenzie pamoja na wengine, walikumbwa na hali mbaya ikiwa pamoja na msongamano wa watu, ukosefu wa mawasiliano, matandiko na taratibu zinazostahili.

Mackenzie amekua akizuiliwa Shimo la Tewa kwa muda wa zaidi ya miezi mitano kwa madai ya mauaji ya jinai eneo la Shakahola, kaunti ya Kilifi baada ya Zaidi ya miili mia moja kupatikana kwenye kaburi la jumla.

Washukiwa hao walilalamika kwa kulazimishwa kurekodi taarifa bila idhini yao ambapo watano wao walipigwa na kulazimishwa kurekodi taarifa zao.

Tume hiyo pia iliona kwamba wafungwa hawakupewa haki ya kuwasiliana na familia zao katika magereza yote matatu kama ilivyoainishwa kisheria na eneo la kutembelea lilizuia mawasiliano na wageni wao.

Walifahamisha tume kwamba wengi wao hawajui mashtaka yanayopendekezwa dhidi yao na hawawezi kujiandaa kwa utetezi wao.

Katika wasia wao, washukiwa hao waliomba kufikishwa mahakamani bila kuchelewa zaidi na kuachiliwa kwa dhamana.

Pia wanataka kuruhusiwa kuwasiliana na wakili wao ili waweze kujipanga kwa utetezi wa kesi inayowakabili.

Tume hiyo ilifanya uchunguzi huo baada ya Hakimu Mwandamizi Mkuu Shikanda kutoa mwelekeo wa madai hayo kuchunguzwa yaliyowasilishwa na Mackenzie kupitia wakili wake Wycliffe Makasembo.

“Mteja wangu hajawai fanyiwa mahojiano wala kusikizwa jambo ambalo ni ukiukaji wa haki zake za kibinadamu,” alisema Bw Makasembo.

Mackenzie aliambia mahakama kwamba anapitia hali ngumu inayomsumbua hata kiakili kwa kutoruhusiwa kuzungumza na mtu yeyote na pia kutokubaliwa kutoka nje ya seli yake.

Pia alidai kuwa hayuko salama katika Gereza la Shimo La Tewa GK na kwamba hakuruhusiwa kunyoa licha ya maombi yake mengi.

Mackenzie alidai kuwa chumba chake kilikuwa na chawa, kunguni na mchwa na alinyimwa ruhusa ya kunyolewa baada ya kutoa ombi zaidi ya mara tano.

Tume baada ya matokeo ya uchunguzi huo, ilipendekeza mahakama kufanya ziara za kila mwezi za usimamizi katika magereza hayo matatu ambapo walalamishi wanazuiliwa.

  • Tags

You can share this post!

Kipa Annette Kundu aendelea kusherehekea ushindi wa Kenya...

Wakulima 750,000 wa chai kupokea maelfu mwezi ujao

T L