• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kipa Annette Kundu aendelea kusherehekea ushindi wa Kenya dhidi ya Cameroon

Kipa Annette Kundu aendelea kusherehekea ushindi wa Kenya dhidi ya Cameroon

NA TOTO AREGE

KIPA Annette Kundu, ambaye alichangia pakubwa katika ushindi wa 4-3 wakati Kenya ilitandika Indomitable Lionesses ya Cameroon anaendelea kusherekea baada ya ushindi huo.

Kwenye mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwakani, Starlets walifanikiwa kuwaondoa Cameroon mashindanoni kupitia mikwaju ya penalti, baada ya mikondo miwili ya mechi kukamilika kwa sare ya 1-1.

Bao pekee la mechi hiyo lilifungwa na kiungo nguvu mpya Cynthia Shilwatso kunako dakika ya 75.

Inafaa kukumbuka kuwa Kenya na Cameroon zimemenyana mara sita sasa, huku Kenya ikikosa kufuzu kwa makala ya tano ya michuano hiyo nchini Nigeria mwaka 2006. Kenya ilifungwa 4-0 mjini Yaounde 5-0 jijini Nairobi mtawalia.

Mwaka 2016, zilikutana katika mechi za kupimana nguvu – jijini Nairobi mnamo Oktoba 22 ambapo Kenya ilifungwa 1-0 na Novemba 6 huko Cameroon ambapo Kenya pia ilifungwa 2-1.

Kenya sasa itamenyana na Botswana katika raundi ya pili ya mchujo mnamo Novemba 27, 2023, na nyumbani Desemba 5, 2023. Botswana ilikuwa imeilaza Gabon kwa jumla ya mabao 10-1 na kufuzu kwa fainali.

Mshindi wa mechi hii atafuzu katika makala ya 15 ya WAFCON nchini Morocco.

Kundu alichangia pakubwa katika ushindi huo wa Jumanne ambapo aliokoa penalti za beki Charlene Meyong na kiungo Claudine Fallone wa Cameroon.

“Nimejawa na furaha kwa ushindi tulioupata kwenye mechi hiyo. Mechi yetu ugenini kama ilivyotarajiwa ilikuwa na changamoto nyingi. Hata hivyo, tulidhamiria kudhihirisha ubabe wetu kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” Kundu alisema Jumanne baada ya mechi.

“Ushindi wetu unatusogeza hatua moja karibu na kufuzu WAFCON. Tumejiandaa kukabiliana na timu yoyote itakayokuja kwetu. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa mashabiki waliojitokeza kutushangilia pale uwanjani Nyayo,” aliongeza Kundu.

Kundu, 26, anachezea klabu ya Ness Atromitou FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Ugiriki.

Mnamo 2018, alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Starlets ikicheza dhidi ya Ghana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ambayo iliishia sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

El Nino: Hofu ya wakazi wa Mukuru-Kayaba jijini Nairobi

Ni kweli Mackenzie anataseka gerezani, tume ya haki yaambia...

T L