• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
NILIKUSALITI, NISAMEHE: Mbunge wa zamani wa Kesses Swarup Mishra anyenyekea kwa Ruto

NILIKUSALITI, NISAMEHE: Mbunge wa zamani wa Kesses Swarup Mishra anyenyekea kwa Ruto

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA mbunge wa Kesses, Bw Swarup Mishra, ameomba msamaha kwa Rais William Ruto na jamii ya Wakalenjin kwa “kuwasaliti” wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita.

Kwenye ujumbe aliotoa Alhamisi, Septemba 21, 2023, muda mfupi baada ya kujiunga na chama tawala cha United Democratic Movement (UDA), Bw Mishra alimrai Dkt Ruto na jamii hiyo “kumsamehe kwa makosa yote aliyowafanyia hapo awali”. Eneobunge hilo liko katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kwenye uchaguzi wa Agosti 9, Bw Mishra alitetea kiti chake kama mwaniaji huru, lakini akashindwa na Bw Julius Ruto wa UDA, aliyezoa kura 32, 839. Bw Mishra aliibuka wa pili kwa kupata kura 21, 404.

Katika taarifa yake, Bw Mishra alisema anaelewa “imani ambayo Wakenya wengi wako nayo kwake”, akiahidi “kuzingatia hekima, uungwana na matamanio ya jamii ya Wakalenjin na Wakenya kwa jumla”.

“Kwa shemeji zangu Wakalenjin, Wakenya na Rais William Ruto, naomba msamaha kwa kosa lolote nililofanya hapo awali,” akaeleza mbunge huyo wa zamani.

Bw Mishra ni miongoni mwa viongozi waliopoteza nyadhifa zao baada ya kusombwa na wimbi la chama cha UDA, lililovuma kote kote katika ukanda huo, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto.

Kando na hayo, mbunge huyo wa zamani alitangaza kuunga mkono utawala wa Rais Ruto, huku akimrai kumpa kazi, akisema yuko tayari kuhudumu katika nafasi yoyote atakayopewa.

“Natangaza wazi kujitolea kwangu kumuunga mkono Rais Ruto na kumsaidia kutimiza mipango aliyo nayo kwa Wakenya. Niko tayari kuhudumu katika nafasi yoyote nitakayopewa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru, mamake wavunja kimya na kumuomboleza shujaa wa Mau...

Wakenya wakisota, kuna Sh28 milioni zimekosa wenyewe...

T L