• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Uhuru, mamake wavunja kimya na kumuomboleza shujaa wa Mau Mau Kirima siku ya mazishi

Uhuru, mamake wavunja kimya na kumuomboleza shujaa wa Mau Mau Kirima siku ya mazishi

Na LABAAN SHABAAN

Kimya cha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kimekuwa na mshindo mkuu miongoni mwa Wakenya siku za hivi karibuni.

Haya ni baada ya kutulia kwa kivumbi cha maandamano dhidi ya utawala wa serikali ya Kenya Kwanza yaliyoongozwa na upinzani, Azimio la Umoja.

Kupoa kwa shinikizo dhidi ya serikali na kushuka kwa mashambulizi dhidi ya familia yake kuliishia kwa rais mstaafu kutoonekana na kutosikika tena hadharani kwa takriban miezi miwili sasa.

Wakati mmoja Rais Mstaafu alikula mori hadharani baada ya familia yake kuagizwa kusalimisha bunduki 25 zilizosajiliwa kwa majina yao kufikia Julai 24, 2023 zilipodhaniwa kutumika katika maafa wakati wa maandamano ya upinzani.

Kabla ya hapo, kulikuwa na kisa ambapo shamba la familia yake la Northlands lilivamiwa, kondoo aina ya Dorper kuibwa na miti kuchomwa kwa kile kilichoonekana kuwa kukithiri kwa uhasama baina ya wanaounga mkono Serikali na wale walio upinzani.

Lakini Ijumaa Septemba 22, 2023 Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Azimio la Umoja amevunja ukimya kwa kumuomboleza na kumuaga shujaa wa Mau Mau mwendazake Muthoni wa Kirima aliyekuwa anafanyiwa mazishi.

Bw Kenyatta na mamake, Mama wa Taifa wa Kwanza Mama Ngina Kenyatta walituma taarifa ya pamoja kuungana na familia, jamaa na marafiki wa mwendazake Muthoni wa Kirima kusherehekea maisha ya shujaa huyo wa vita vya uhuru.

Kupitia taarifa kwa familia iliyoathiriwa, Bw Kenyatta amemtaja Bi Muthoni wa Kirima kuwa mzalendo, shujaa mkubwa na mmoja wa wapiganiaji uhuru wanaoheshimiwa sana.

“Alama zake za miguu hususan msituni zilikuwa muhimu sana kusaidia viongozi kama yeye vitani kukata minyororo ya ukoloni kwa haki za Wakenya kisiasa, kijamii na kuimarisha uchumi kufanikisha nchi ipate uhuru na ustawi,” alieleza akiongeza kuwa marehemu hatakumbukwa tu kwa ujasiri wake bali pia kwa bidii alipohudumia Kenya.

Naye Mama Ngina Kenyatta alisema, “Ninathamini kumbukumbu na furaha tulipokutana na Bi Muthoni wa Kirima na kusimuliana hadithi nyingi pamoja hivi karibuni. Ninashukuru Mungu kwa fadhila na heshima ya kumjua na kushiriki kumbukumbu za wakati mgumu wa nchi kipindi cha serikali ya ukoloni.”

Mama Ngina Kenyatta akimnyoa nywele Muthoni Kirima. Picha|Maktaba

Marehemu aliyezikwa Septemba 22, 2023 nyumbani kwake Tetu, Kaunti ya Nyeri alifariki Septemba 5, 2023 akiwa na umri wa miaka 92 katika hospitali moja eneo la Pangani jijini Nairobi baada ya kukumbwa na matatizo ya kiafya.

Bi Muthoni alikuwa msaidizi wa kibinafsi wa marehemu Dedan Kimathi katika vita vya uhuru.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume mpenzi wangu alichovya nje nikamtema, sasa nahisi...

NILIKUSALITI, NISAMEHE: Mbunge wa zamani wa Kesses Swarup...

T L