• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
Nyota wa ‘Stella Wangu’ adaiwa kutelekeza mama

Nyota wa ‘Stella Wangu’ adaiwa kutelekeza mama

NA LUCY MKANYIKA

MWIMBAJI mashuhuri Freshley Mwamburi, amejikuta lawamani kwa madai ya kumtelekeza mamake, Bi Sophy Mkakina.

Katika kijiji chao kilicho Kishushe, Kaunti ya Taita Taveta, Bi Mkakina, 72, anaeleza kwamba Freshley aliyejizolea umaarufu kimataifa kwa wimbo wake wa ‘Stella’, hajakuwa akimshughulikia na wala hajamtembelea nyumbani kwa zaidi ya miaka 20.

Bi Mkakina anaonekana mnyonge na anasema anatatizika sana kwa uzee na magonjwa huku akiwa mpweke. Sasa anategemea majirani kumsaidia kupata chakula na maji.

“Awali nilikuwa najitegemea hata ingawa nilikuwa naishi peke yangu, hadi nikawa mgonjwa na singeweza tena kufanya vibarua ili kujikimu,” akasema.

Kulingana naye, alitaabika sana kumlea Freshley ambaye ni mwana wake wa pekee kwa kufanya kazi za nyumbani Mombasa.

Matatizo hayo yalimsababisha Freshley kukosa karo ya kuendeleza shule ya upili kwa vile mamake hangegharimia.

“Baada ya muda nilikuwa mgonjwa nikalazwa katika Hospitali Kuu ya Pwani mjini Mombasa. Alikuja hata kuniona ndipo akanieleza alianza kusomea muziki,” akasema.

Aliporuhusiwa kwenda nyumbani ndipo alirudi kijijini kwao Kishushe, ambapo kakake alimgawia kipande cha ardhi na kumjengea nyumba ndogo.

Bi Mkakina anasema katika miaka ya awali, hakugundua mtoto wake alikuwa na kipaji cha muziki lakini alishukuru kwamba angeweza kujichumia riziki.

Hata hivyo, kipaji hicho ndicho kilianza kumsababisha Freshley kusonga mbali na mamake hasa alipoenda Nairobi.

“Kuna wakati hata nilikuwa bado namsaidia kifedha kwa vile muziki ulikuwa haumlipi vyema. Hapa kijijini nilikuwa Napata pesa kidogo kutoka kwa vibarua kama vile kuchunga mifugo ya kakangu au kulima shambani. Sasa sina nguvu kufanya hayo yote na ninalazimika kuombaomba,” akasema.

Alieleza kuwa, ombi lake kuu ni kwa mwanawe kurudi nyumbani ili aonyeshwe shamba la ekari mbili ambalo mamake alirithi kutoka kwa kakake kama bado angali hai.

“Wakati mwingine yeye hunipigia simu na huwa namwambia nataka kumwona. Namtaka pia amlete mke wake kwa sababu nasikia ameoa lakini hajawahi kuniletea mke wake,” akasema.

Wakati wa mwisho walipoonana, ilikuwa ni miaka miwili iliyopita katika mazishi ya jamaa wao Windanyi ambapo inasemekana aliahidi kwenda nyumbani kwao lakini hajawahi kuonekana.

“Sijui nini ilimfanya hadi akanitelekeza. Sina haja na pesa zake. Namtaka tu aje nyumbani kabla Mungu anichukue,” akasihi.

Katika mahojiano na Taifa Leo, mwimbaji huyo alikana vikali madai ya mamake akisema yanalenga kumharibia sifa.

Alidai kuwa, ana mipango kabambe kwa mamake huku akisisitiza amekuwa akimtunza. Lakini alikataa kuulizwa maswali mengine zaidi kuhusu hali ya mamake.

“Najua ile mipango niliyo nayo kwa mamangu. Kuna watu wanataka kuniharibia sifa kwa sababu sikuwasaidia,” akasema.

Bi Janet Ngele, jirani na mamake, alisema aliwahi kumpigia simu Freshley mara kadha kumwambia mamake anahitaji usaidizi.

“Nilikuwa nikimpigia simu, anasema atakuja lakini haji. Jumbe nilizomtumia hazikujibiwa. Niliacha kuwasiliana naye nikamwambia mamake asijali kwani mwanawe atakuja siku moja,” akasema Bi Ngele.

Kaimu Chifu wa eneo la Kishushe, Bi Ethel Mosa, alisema wamejaribu sana kumtafuta Freshley lakini hawajafua dafu.

Alisema Bi Mkakina hajasajiliwa kwa mpango wa kupokea pesa za wazee kutoka kwa serikali kwa sababu umri wake haukubainika wakati alipohojiwa kwa usajili.

“Wanakijiji wamejaribu kumsaidia kwa kumjengea nyumba ndogo. Tutahakikisha atapokea chakula cha msaada wakati kitakapoletwa,” akasema Bi Mosa.

Aliomba serikali iongeze watu kwa mpango wa misaada ya wazee hasa wakati huu ambapo wengi wanakumbwa na njaa.

  • Tags

You can share this post!

Wafanyakazi sasa kujilipia gharama ya matibabu jijini

Shule kufungwa Tiaty kwa ukosefu wa chakula

T L