• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ombi la Mackenzie kuonja uhuru lilivyogonga mwamba

Ombi la Mackenzie kuonja uhuru lilivyogonga mwamba

NA WAANDISHI WETU

JARIBIO la mhubiri Paul Mackenzie, kutaka uhuru wake uligonga mwamba Jumanne mahakama ilipotupa nje ombi hilo.

Mawakili wa mshukiwa huyo, ambao ni Bw George Kariuki na Elisha Komora, walisema alishafungwa kwa muda mrefu hivyo basi alistahili kupewa bondi ya kuzuia kukamatwa kwake. Amekuwa kizuizini kwa siku 14.

Walitoa ombi hilo wakati Upande wa Mashtaka ulifunga kesi ya awali dhidi yake na washukiwa wenzake wanane, ili kupata fursa ya kumshtaki kwa madai mapya mazito.

Bw Mackenzie amedaiwa kuhusika kwa vifo vya watu zaidi ya 110 Shakahola, Kaunti ya Kilifi, wanaoaminika walikuwa waumini wa dhehebu lake ambao aliwashawishi kufunga kula na kunywa hadi wafe ili waende mbinguni.

Viongozi wa Mashtaka, Bi Vivian Kambaga, Alice Achola na Sylvia Ole’Suke, waliambia mahakama ya Malindi kuwa wangependa kupeleka kesi yake katika mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi ambazo zitafunguliwa dhidi yake na washukiwa wenzake wanane.

“Upelelezi unaendelea na hauhusu tu mashtaka ya mauaji na mengine yaliyoletwa katika mahakama hii awali. Tunaangalia mashtaka kuhusu mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu, na ulanguzi fedha. Huu ni upelelezi mgumu na kwa hivyo, hatuwezi kushinikizwa kuukamilisha kwa siku moja… maisha yamepotezwa,” Bi Achola akaambia mahakama.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Malindi, Bi Ivy Wasike, aliungama kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yanayonuiwa dhidi ya mhubiri huyo, akafunga kesi hiyo.

Bw Mackenzie na washukiwa wenzake walikamatwa upya kabla kuondoka mahakamani Malindi wakapelekwa Mahakama ya Shanzu ambapo alitarajiwa kusomewa mashtaka upya. Walikuwa bado wanasubiri kusomewa mashtaka wakati gazeti hili lilipoenda mtamboni.

Akiwa mahakamani, mhubiri huyo alionekana mchovu akisemezana na washukiwa wenzake mara kwa mara. Awali asubuhi, mkewe pia alikuwa amekamatwa na polisi.

Hayo yalijiri huku mhubiri wa kanisa la New Life, Bw Ezekiel Odero, akirudishwa seli hadi kesho ili kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi wao.

Katika kesi hiyo, polisi walipata pigo baada ya mahakama kukataa ombi la kutaka azuiliwe kwa siku 30 ili wakamilishe uchunguzi wao.

Mahakama ya Shanzu iliamua kuwa, akae kizuizini kwa siku saba pekee ambazo zinahesabiwa kuanzia Aprili 27 alipokamatwa. Hivyo basi, atatakiwa kurudishwa mahakamani kesho, Mei 4.

Polisi wanamchunguza Bw Odero na kanisa lake lililo Mavueni, Kaunti ya Kilifi, kuhusu madai kwamba vifo vimekuwa vikitokea katika kanisa hilo, huku wakitaka pia kubainisha kama kuna uhusiano wowote kati ya kanisa lake na dhehebu la Bw Mackenzie.

RIPOTI ZA WACHIRA MWANGI, BRIAN OCHARO Na ALEX KALAMA 

  • Tags

You can share this post!

Uhuru matatani Sabina ‘akihepa’ na Jubilee Party

Maandamano ya Azimio yalivyozimwa

T L