• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Omingo Magara alia ‘kucharazwa’ na baridi, amsihi Rais Ruto kumkumbuka

Omingo Magara alia ‘kucharazwa’ na baridi, amsihi Rais Ruto kumkumbuka

NA WYCLIFFE NYABERI

MBUNGE wa zamani wa Mugirango Kusini, Omingo Magara amesema anajutia uamuzi wake kugura chama cha UDA na kujiunga na Jubilee kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Magara sasa anamtaka Rais William Ruto amkumbatie na amsamehe kwani kibaridi cha kuwa nje ya serikali kinamuumiza.

Kufuatia ziara ya Rais Ruto eneo la Kisii mnamo Jumamosi, Julai 22, 2023, Bw Magara aliwaacha wengi vinywa wazi aliposema anajutia kukaidi rai ya Dkt Ruto kumtaka asalie UDA.

“Nakumbuka kwa ufasaha hapa (Etago) ndiko ulipotuorodhesha mimi na Machogu…Ukasema nikae pande hii na Machogu akae pande ile… Lakini mheshimiwa nilikukaidi na majuto ni mjukuu. Lakini cha muhimu, kuna msemo unasema; Hata kama hutaki mama yako aolewe pahali fulani, atakayeoa mamako ndiye babako. Sasa kama amechukua mama si tujiunge naye tufanye kazi,” Bw Magara alisema huku umati mkubwa uliohudhuria hafla hiyo ukiangua kicheko.

Bw Magara alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha UDA baada ya ndoa ya kisiasa kati ya Dkt Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kuingia doa.

Aliteuliwa kuwa mwekahazina wa chama hicho tawala, lakini siku chache kabla ya uchaguzi mkuu 2022 kufanyika, Bw Magara aligura UDA na kukimbilia Jubilee, akilalamikia kwamba chama hicho chenye nembo ya wilibaro hakina demokrasia.

Chama cha Jubilee kilimpa tikiti kuwania useneta Kisii lakini alibwagwa na aliyekuwa mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Bw Richard Onyonka.

Bw Onyonka alizoa kura 173, 189 dhidi ya kura 121, 339 za Bw Magara.

Nafasi ya UDA aliyoiacha Bw Magara, ilitwaliwa na mbunge wa sasa wa Kitututu Chache Kaskazin, Japheth Nyakundi.

 

  • Tags

You can share this post!

Mwili wa afisa wahamishwa mipango ya mazishi ikianza

Masaibu: Bloga wa Azimio Pauline Njoroge akamatwa kwa madai...

T L