• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Pigo kwa Sonko IEBC ikimzidi ujanja raundi ya kwanza

Pigo kwa Sonko IEBC ikimzidi ujanja raundi ya kwanza

PHILIP MUYANGA NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi, Bw Mike Mbuvi Sonko, alipata pigo Jumanne Mahakama ya Mombasa ilipokataa ombi lake la kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iagizwe kumwidhinisha kuwania ugavana Mombasa wakati kesi zake zinapoendelea kusikilizwa.

Bw Sonko, mwanachama wa Wiper, alikuwa amewasilisha kesi kadha mahakamani na kwa jopo la kutatua malalamishi katika IEBC kupinga uamuzi wa tume hiyo kuzima azma yake.

Jaji John Mativo, alisema ingekuwa hatari kwa mahakama kutoa agizo aina hiyo kwa sasa kwani pande tofauti hazijasikizwa na pia huenda agizo aina hiyo ikahitilafiana na kesi nyinge zinazohusiana na suala hilo hilo.

Wakati uo huo, IEBC imepinga kesi hiyo ya Bw Sonko ikisema mahakama haina mamlaka ya kusikiza malalamishi yaliyotolewa.

Kupitia kwa wakili Edwin Mukele, tume hiyo ilisema suala hilo lilifaa kusikizwa mbele ya jopo la malalamishi la IEBC.

Jaji Mativo aliagiza kuwa, suala lililoibuliwa na IEBC kupinga mamlaka ya mahakama kusikiza kesi hiyo litakuwa la kwanza kuamuliwa.

Bw Mukele aliomba kesi iahirishwe, akisema alihitajika kusafiri Nairobi kuhudumia jamaa wake aliyeugua. Kesi hiyo iliahirishw ahadi Ijumaa.

Katika malalamishi yake, Bw Sonko anataka uamuzi wa IEBC na Bw Chebukati uliotangazwa Juni 4, kwamba hastahili kuwania kiti cha kisiasa kwa vile alibanduliwa mamlakani Nairobi, ubatilishwe.

Anataka pia uamuzi wa mkuu wa uchaguzi Mombasa kukataa kumwidhinisha kuwania ugavana Mombasa ubatilishwe na mahakama.

Kulingana naye, suala la kuwa hafai kuwania kiti cha kisiasa kwa msingi wa kung’atuliwa mamlakani kwa sababu za kimaadili, halina msingi kwa vile amekata rufaa dhidi ya hatua hiyo katika Mahakama ya Juu.

Bw Sonko analalamika kuwa, uamuzi wa tume ya uchaguzi kumzuia kuwania ugavana Mombasa unakiuka haki zake kwa ile ulifanywa kabla apewe nafasi ya kujieleza.

“Hili ni suala linalohitajika kuamuliwa kwa haraka kwa vile lina umuhimu mkubwa kwa umma na pia, itakuwa kwa manufaa ya haki kwa sababu ya jinsi ratiba ya uchaguzi ilivyo,” akasema Bw Sonko.

Mwanasiasa huyo amewakosoa pia IEBC na maafisa wake akisema walikosea na kumdhulumu kwani kuna wanasiasa wengine waliohukumiwa ilhali wamekubaliwa kuwa wagombeaji katika uchaguzi Agosti kwa sababu walikata rufaa dhidi ya hukumu zao.

Amezidi kudai kuwa, maamuzi yanayofanywa na mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, dhidi yake yanachochewa na shinikizo kutoka nje ya tume hiyo.

“Maamuzi ya mshtakiwa wa pili (Bw Chebukati) yanatofautiana na mahitaji ya mamlaka ya afisi yake kufanya maamuzi kwa njia huru, bila mapendeleo wala uoga,” akasema Bw Sonko, katika mawasilisho yake.

Malalamishi sawa na hayo yaliwasilishwa kwa jopo la IEBC la kusikiza malalamishi Nairobi, ambapo aliandamana na kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka.

IEBC imejitetea ilikataa kumwidhinisha kwa kutowasilisha cheti chake halisi cha shahada ya digrii, chapa ya cheti hicho iliyopigwa muhuri na chuo kikuu alikosomea, na ukiukaji wa Ibara 75 ya Katiba.

Sehemu hiyo ya Katiba ndiyo ilitumiwa kumng’oa mamlakani Nairobi.

IEBC imezidi kujitetea kuwa, haikupokea agizo lolote kutoka kwa mahakama kwamba Bw Sonko aidhinishwe, jinsi anavyodai.

Wiper inataka jopo hilo liamue kuwa Bw Sonko aliwasilisha stakabadhi zote zilizohitajika na IEBC Juni 7, na kwamba mkuu wa uchaguzi Mombasa alikosea kwa kukataa kumwidhinisha.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke asakwa kwa madai ya kuhepa na gari la mpenzi

Kalonzo apata nguvu mpya Ukambani kote

T L