• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kalonzo apata nguvu mpya Ukambani kote

Kalonzo apata nguvu mpya Ukambani kote

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ameanza kupata nguvu mpya katika ngome yake ya kisiasa ya Ukambani baada ya kuzika tofauti zake na mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga na kurejea katika muungano huo.

Japo aliingia katika muungano huo kuchelewa, Bw Musyoka ameteka kampeni za Bw Odinga katika eneo hilo huku viongozi walioungana na Bw Odinga mapema wakigeuzwa kuwa watazamaji.

Bw Musyoka alijiondoa katika Azimio la Umoja One Kenya kwa muda alipokosa kuteuliwa mgombea mwenza wa Bw Odinga na akatangaza kuwa angegombea urais kwa tikiti ya chama cha Wiper.

Hii ilimfanya akashifiwe vikali na viongozi wa vyama tanzu vya muungano huo vyenye mizizi Ukambani wakiwemo Charity Ngilu (Narc), Nzioka Waita (CCU) na Profesa Kivutha Kibwana (Muungano) waliomlaumu kwa kutaka kuyumbisha meli ya Azimio eneo la Ukambani.

Watatu hao, miongoni mwa wengine, walikuwa wakimpigia debe Bw Odinga wakati Bw Musyoka alikuwa akitapatapa.

Bw Musyoka aliondoa azima yake ya kugombea urais baada ya wiki mbili na kukubali wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri aliotengewa na Bw Odinga Azimio ikishinda urais na kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Baada ya kurejea katika Azimio, Bw Musyoka ameandamana na Bw Odinga kuhutubia mikutano kadhaa ya kampeni katika kaunti za Machakos na Makueni ambayo inaendelea kumsawiri kama kiongozi wa kampeni za Azimio eneo hilo ambapo chama chake cha Wiper kina wafuasi wengi.

“Ni kweli, kurejea Azimio kumempa Kalonzo nguvu mpya na kumfufua kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Kumbuka chama chake ndicho kikubwa Ukambani na ndio sababu anang’aa katika mikutano yake na Bw Odinga kuliko viongozi wa vyama vingine vyenye mizizi eneo hilo,” akasema mchanganuzi wa siasa Ukambani Dkt Nicholas Syano.

Anasema Bw Musyoka ana historia ya miaka mingi na Bw Odinga na ndio sababu waziri mkuu huyo wa zamani alichelewesha kampeni zake eneo hilo hadi makamu rais huyo wa zamani akarudi katika Azimio.

Kung’aa kwake katika mikutano ya kampeni za Bw Odinga, kumekasirisha viongozi wengine wa muungano huo ambao wanamlaumu kwa kupigia debe wagombeaji wa chama chake cha Wiper ilhali kuna wa vyama tanzu mbalimbali vya Azimio.

Tayari, mzozo unatokota katika kaunti ya Machakos, baada ya Bw Musyoka kumtaka Bw Waita kujiondoa katika kinyanganyiro cha ugavana na kumwachia Bi Wavinya Ndeti wa chama cha Wiper.

Kulingana na Bw Waita, Bw Musyoka anasahau kwamba aliingia Azimio kuchelewa na anafaa kuacha wapigakura kuamua viongozi wanaotaka wawaongoze.

“Bw Musyoka anafaa kufahamu kwamba, hana kura ya Machakos na kuacha wapigakura wa Machakos kuamua wanayetaka awaongoze,” asema Bw Waita.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuungana tena kwa Bw Musyoka na Bw Odinga kunafufua ushirika wao wa tangu uchaguzi mkuu wa 2013.

“Awali, Bw Musyoka alionekana kufifia kwa kuwa hakuwa ameamua kuungana na Bw Odinga. Hawa ni watu ambao wamekuwa pamoja tangu 2013 na kurudi kwa kiongozi wa Wiper katika Azimio kumempa nguvu ambazo wapinzani wake walidhani wamempokonya,” asema Bw Syano.

Mchanganuzi huyu anasema hii inaonekana wazi na umati unaohudhuria mikutano ya kampeni za Bw Odinga anakoandamana na Bw Musyoka eneo la Ukambani.

Bw Musyoka ndiye mwanasiasa wa Ukambani ambaye Bw Odinga ametengea wadhifa mkubwa katika serikali iwapo Azimio itashinda urais na kuunda serikali kwenye uchaguzi mkuu ujao.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa Sonko IEBC ikimzidi ujanja raundi ya kwanza

UFUGAJI: Wafugaji watafuta njia za kumudu gharama ya lishe

T L