• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
Polisi ashtakiwa kwa kuitisha hongo kutoka kwa mhudumu wa bodaboda

Polisi ashtakiwa kwa kuitisha hongo kutoka kwa mhudumu wa bodaboda

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

KAMANDA mmoja wa polisi Jumatano alishtakiwa katika mahakama moja ya Makueni kwa kosa la kupokea hongo ya Sh5,000 kutoka kwa mhudumu wa bodaboda miezi saba iliyopita.

Bw Henry Mutunga ambaye ni Naibu Kamanda wa Wadi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Khwisero, Kaunti ya Kakamega hata hivyo alikana kutenda kosa hilo na akaachiliwa huru kwa dhamana ya Sh150,000 pesa taslimu au mdhamini wa Sh300,000.

Kulingana na stakabadhi ambazo Taifa Leo iliona, mshukiwa aliamuru kukamatwa na kuzuiliwa kwa Joseph Kioko Mutuku mnamo Septemba 14, 2020, alipokuwa akitekeleza sheria za kafyu.

Wakati huo alikuwa akihudumu kama Kamanda wa Wadi katika Kituo cha Polisi cha Mukuyuni kilichoko Kaunti ya Makueni.

Bw Mutunga alidai kuwa Mutuku aliiba pikipiki ya thamani ya Sh85,000 na kuwa na misokoto 10 ya bangi ya thamani ya Sh1,000.

Bw Mutuku aliwasilisha malalamishi yake kwa maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ambao waliweka mtego.

Miezi saba baadaye mhudumu huyo wa bodaboda alikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Capitol Hill.

Familia ya Mutuku ilimsuta kamanda huyo kwa kuitisha na kupokea hongo kutoka kwa Jeremiah Mutuku, ambaye ni kakake mwanabodaboda huyo, ili aachiliwe huru.

Bw Mutunga hakufunguliwa mashtaka alipofikishwa mahakamani Jumanne.

“Mnamo Septemba 14, 2020, ukiwa afisa wa kituo cha polisi cha Mukuyuni ndani ya Kaunti ya Makueni uliitisha na kupokea hongo ya Sh5,000 kutoka kwa kakake Joseph Kioko Mutunga, ambaye alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa katika kituo kwa kosa la ulaghai,” ikasema hati ya mashtaka iliyotolewa Jumanne.

You can share this post!

FRENCH CUP: PSG yaingia nusu-fainali baada ya kuponda...

Real Madrid wachabanga Cadiz na kupaa hadi kileleni mwa...