• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Polisi wazidisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Chiloba

Polisi wazidisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Chiloba

NA BARNABAS BII

MAKACHERO kutoka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) wamewakamata washukiwa wengine zaidi wanaohusishwa na mauaji ya mwanaharakati wa haki za mashoga Edwin Kiptoo almaarufu Chiloba.

Haya yanajiri huku jamaa wa familia yake wakipanga hafla ya mazishi Alhamisi nyumbani kwao Sergoit, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Afisa wa upelelezi katika Kaunti ya Uasin Gishu Peter Kimulwa jana Jumapili alisema washukiwa wakuu wamekamatwa na kuwa uchunguzi kuhusiana na kisa hicho cha mauaji umekamilika.

“Washukiwa wakuu kufikia sasa wamezuiliwa na kuna kesi thabiti ya kuwafungulia kortini. Hatutarajii kuwakamata watu zaidi isipokuwa vinginevyo,” alisema Bw Kimulwa kupitia simu.

Washukiwa watano wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo huku makachero wakikusanya ushahidi zaidi na kuimarisha kesi.

Washukiwa hao ambao Jumatatu iliyopita walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu, Richard Odenyo wamewekwa kizuizini kwa siku 21 ambapo kesi hiyo itatajwa Januari 31.

Mshukiwa mkuu katika mauaji hayo Jacktone Odhiambo mnamo Ijumaa iliyopita aliwaongoza wapelelezi wa DCI katika maeneo matatu katika juhudi za kufuatilia nyakati za mwisho za mkereketwa huyo wa wasenge (LGBTQ) na mwanafasheni.

Bw Odhiambo aliyefungwa pingu na kuvishwa gauni jeupe aliwaongoza wapelelezi kwa nyumba yake marehemu Chiloba katika eneo la Noble Breeze, Chebisaas karibu na Chuo Kikuu cha Eldoret ambapo mwendazake alikuwa anasomea.

Aidha, makachero hao walizuru kijiji cha Mokombet ambapo mwili wa Bw Chiloba uliokuwa umeanza kuoza ulikuwa umefungiwa ndani ya sanduku la chuma na kutupwa kando ya barabara ya Kipenyo – Kaptinga, eneo la Kapsaret, Uasin Gishu.

Walienda vilevile katika eneo la Kahoya nyumbani kwa wazazi wake Odhiambo ambaye baba yake anasemekana kuwa mhubiri mashuhuri na mwenyekiti wa Nyumba Kumi.

Wapelelezi walipata kifurushi cha nguo za mwendazake katika boma hilo. Makachero watakusanya picha za kamera za CCTV katika hoteli ya Tamasha Lounge ambapo Odhiambo na marehemu Chiloba walionekana kwa mara ya kwanza wakicheza densi na marafiki walipokuwa wakiukaribisha Mwaka Mpya.

“Tutachukua picha zilizorekodiwa na CCTV katika hoteli ya Tamasha Lounge ili zitusaidie kutambulisha watu zaidi walioonekana mara ya mwisho na marehemu,” alisema Mkurugenzi wa DCI anayesimamia uchunguzi unaohusu visa vya mauaji, Bw Martin Nyuguto.

  • Tags

You can share this post!

Salat aingia Kenya Kwanza rasmi

Nafasi za Kidato cha Kwanza kujulikana leo Jumatatu

T L