• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Raia waelimishwe kuhusu kitengo cha kuripoti polisi

Raia waelimishwe kuhusu kitengo cha kuripoti polisi

TANGU 2013, kumekuwepo na Kitengo cha Kushughulikia Malalamishi Ndani ya Kikosi cha Polisi (IAU) ambacho hupokea na kuchunguza madai yanayotolewa na wananchi dhidi ya maafisa wa polisi.

Kitengo cha IAU kiliundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 87 cha Sheria ya Huduma ya Polisi ya 2011.Kitengo hicho hupokea malalamishi kutoka kwa Mkenya yeyote ambaye amedhulumiwa au kukerwa na afisa wa polisi kwa kutuma arafa, barua pepe, kwenda afisini au kupiga simu.

Baada ya kukamilisha uchunguzi kuhusiana na malalamishi hayo, IAU hutuma ripoti na mapendekezo yake kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Tume ya Huduma ya Polisi (NPS) au kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

IAU pia inastahili kumfahamisha mlalamishi kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya afisa husika.Ripoti ya IAU ya 2020 inaonyesha kuwa asilimia 40 ya malalamishi dhidi ya maafisa wa polisi huwasilishwa na wakazi wa jijini Nairobi.

Kati ya malalamishi 1,043 yaliyowasilishwa mwaka jana dhidi ya maafisa fulani wa polisi, kituo cha IAU kilipokea asilimia moja kutoka eneo la Kaskazini Mashariki, Magharibi (asilimia nne), Pwani (asilimia nane) na Nyanza (asilimia tisa).

Kaunti zilizowasilisha chini ya malalamishi matano 2020 ni Narok, Samburu, Garissa, Baringo, Wajir, Tharaka Nithi, Elgeyo Marakwet, Lamu, Pokot Magharibi na Tana River.Asilimia 78 ya malalamishi yalikuwa dhidi ya Kenya Polisi (KPS), maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) asilimia 14 na Polisi wa Utawala (AP) – asilimia tano.

Jumla ya malalamishi 849 yalitoka kwa wananchi, 168 yalipitia kwa maafisa wengine wa polisi na 26 yalitoka kwa watu wasiojulikana. Asilimia 75 ya wananchi wanaolalamika kudhulumiwa na polisi walikuwa wanaume.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, madai yanayowasilishwa kwa IAU yamekuwa yakiongezeka tangu 2017.

Kwa mfano, mnamo 2017 IAU ilipokea jumla ya madai 855, 2018 kitengo hicho kilipokea lalama 950, 2019 kulikuwa na 1,139 na mwaka jana 1043. Ripoti inasema mwaka jana idadi ya malalamishi ilipungua ikilinganishwa na 2019 kwa sababu idadi kubwa ya watu walijifungia majumbani kutokana na janga la virusi vya corona.

Kuwepo idadi ndogo ya malalamishi katika baadhi ya maeneo, kunatokana na sababu mbalimbali.Kwanza, hiyo ni ithibati kwamba Wakenya wengi hawana ufahamu kuhusiana na uwepo wa kitengo cha IAU.

Pili, wananchi wanaogopa kuripoti kwa kuhofia kuandamwa na maafisa waliowadhulumu.Tatu, baadhi ya watu pia hawaoni haja ya kuripoti kwa sababu wanaamini kwamba wahusika hawatachukuliwa hatua yoyote. Hilo linatokana na ukweli kwamba kati ya malalamishi 1,043 yaliyopokelewa mwaka jana, 533 hayajashughulikiwa.

Kwa mfano, ripoti hiyo, inaonyesha kuwa mwaka jana kulikuwa na mtu mmoja pekee ambaye aliripoti kusingiziwa makosa ‘bandia’ na afisa wa polisi, watu 13 walilalamikia kutiwa seli kinyume cha sheria na maafisa 85 walidaiwa kupokea hongo.Katika mitandao ya kijamii kumekuwa na malalamishi tele kuhusu maafisa wa polisi wanaotia watu pingu kiholela bila kufanya makosa na kuomba hongo.

Lakini malalamishi hayo hayafikii IAU.Idara ya polisi inafaa kuwaelimisha Wakenya kuhusu jinsi ya kuwasilisha malalamishi yao kwa kitengo cha IAU ili maafisa wabaya wanaoharibu sifa ya kikosi waadhibiwe. Vilevile, malalamishi yanapowasilishwa yashughulikiwe kwa haraka.

  • Tags

You can share this post!

Raia waelimishwe kuhusu kitengo cha kuripoti polisi

Walimu hawana budi kusubiri miaka 2 bila nyongeza