• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Walimu hawana budi kusubiri miaka 2 bila nyongeza

Walimu hawana budi kusubiri miaka 2 bila nyongeza

Imetokea kama jambo la kushangaza kwa walimu kutangaziwa kuwa hakutakuwa na nyongeza ya mishahara kwa muda wa miaka miwili ijayo.

Hili lilitangazwa na Tume ya Kuajiri Walimu nchini, TSC. Kulingana na TSC, jambo hili linatokana na sababu kuwa Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini, SRC, ilitangaza kusitishwa kwa nyongeza za mishahara kwa muda wa miaka miwili kwa watumishi wote wa umma.

Mwenyekiti wa Tume hiyo ya SRC Bi. Lyn Ngetich akitangaza jambo hili hapo Juni 17 mwaka huu alisema kuwa hali ngumu ya uchumi nchini ambayo imesababishwa na mkurupuko wa Covid-19 imeliweka taifa hili pabaya.

Uchumi wa nchi umezoroteka kwa kiasi kikubwa na itabidi watumishi wote wa umma wavumilie kwa miaka miwili bila nyongeza ya mishahara.Kwa walimu, hili ni suala ambalo wanahitaji kulielewa na kukubali bila malalamishi yoyote hasa ikizingatiwa kuwa kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miezi tisa ambapo hawakuwa kazini waliendelea tu kupata mishahara yao kikamilifu.

Hivi ni kusema kuwa makubaliano ambayo vyama vya KUPPET na KNUT vilikuwa vinataka yatekelezwe yatasubiri kwa muda wa miaka miwili hadi mwaka wa 2023. Hata hivyo, TSC kupitia kwa Bi Nancy Macharia ilisema kuwa marupurupu mengine kama vile yale ya kupata likizo ya kujifungua na mengineyo yataelendelea kulipwa.

Hii ni afueni kwa walimu kwani wataweza kuendeleza maisha yao kikamilifu bila wasiwasi.Jambo la muhimu ambalo walimu wanafaa kukumbuka ni kuwa, kuna watumishi wengi sana wa umma ambao walipoteza kazi zao kabisa na wengine wengi wakapunguziwa mishahara kwa kiwango kikubwa.

Aidha mashirika mengine yasiyokuwa ya kiserikali hayajasazwa katika kuchukua hatua ya kuwapiga kalamu baadhi ya wafanyakazi wake na kupunguzia wengine mishahara yao.Huku hayo yakijiri, walimu pia wanahitaji kukumbana na changamoto zaidi za kuhakikisha kuwa ugonjwa wa Covid-19 hauwafikii au kupenya katika shule zao.

Juma lililopita, ugonjwa huu uliripotiwa kuwapata wanafunzi 99, walimu wanne na mfanyakazi mwengine mmoja katika shule ya upili ya Muruku, kaunti ya Laikipia. Wanafunzi hao na walimu wao waliwekwa katika karantini huku Wizara ya Afya ikiingia shuleni humo kuweza kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo kwa wanafunzi wengine na wanajamii wa eneo hilo.

Kutokana na changamoto hizi na nyingine ambazo zinakumba taifa letu changa kwa wakati huu, hapana shaka kuwa Tume ya kuajiri walimu nchini, TSC ni sharti iupokee wito wa Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini, SRC wa kutoongeza mishahara kwa kipindi kilichotajwa cha miaka miwili. Ni vyema walimu wakubali wito huu kwa moyo mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Raia waelimishwe kuhusu kitengo cha kuripoti polisi

Polio: Wazazi wahimizwa kuwapeleka watoto wao kwa chanjo