• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
RISASI YA SITA? Familia ya Raila yasisitiza hatastaafu siasa

RISASI YA SITA? Familia ya Raila yasisitiza hatastaafu siasa

Na GEORGE ODIWUOR

FAMILIA ya Jaramogi Oginga Odinga imeanzisha mjadala mpya kuhusu ubabe wa kisiasa Luo Nyanza baada ya dada mdogo wa Raila Odinga, Ruth Odinga, kushikilia kuwa kiongozi huyo wa upinzani hatastaafu siasa.

Huku akimtetea kakake kutokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kwamba anapaswa kustaafu siasa, Mbunge huyo Mwakilishi wa Kisumu alishikilia kuwa kiongozi huyo wa Azimio angali miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini.

Kauli yake inaonekana kukinzana na ya msemaji wa familia ya Jaramogi, Oburu Oginga, ambaye majuzi alidokeza kuwa kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi ndiye anatosha kumrithi Bw Odinga kama kiongozi wa kisiasa eneo la Luo Nyanza.

Lakini Bi Odinga alisema kuwa hamna mwanasiasa eneo hilo mwenye sifa zinazoweza kulinganishwa na za kakake huku akiwataka wanasiasa wengine kutoka eneo kusaka ushauri kutoka kwa kiongozi huyo wa ODM.

“Hakuna mtu anayeweza kuwa Rais kutoka eneo hili isipokuwa Raila. Nimetafuta yule mwenye sifa zinazoshahibiana na zake na sijaona yeyote,” akasema.

Bi Odinga alisema hayo Alhamisi Septemba 14, 2023 katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Mirogi katika eneo bunge la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay.

Alimshauri Raila asiitikie presha kutoka kokote za kumtaka astaafu kutoka siasa.

Alikuwa amehudhuria shughuli kwa jina, “Mama County Back to School” iliyodhaminiwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay Joyce Osogo na kuhudhuriwa na Gavana wa kaunti hiyo Gladys Wanga.

Bi Odinga alieleza kuwa, Raila mwenye umri wa miaka 78, anazo sifa za kumwezesha kuliongoza taifa hili licha ya kujaribu mara tano na kufeli.

“Hakuna mtu kutoka eneo hilo la Nyanza anayeweza kumrithi na kuwania urais kisha ashinde.

Bi Odinga alitoa wito kwa watu kutoka Nyanza kumuunga mkono Waziri Mkuu huyo wa zamani akisema anao uwezo wa “kukomboa” jamii za eneo hilo.

“Raila ndiye anafaa kuungwa mkono na viongozi wa eneo hili wanafaa kuendelea kufanya hivyo,” akaeleza.

Dkt Oginga, ambaye ameondoa kauli yake ya awali, ameeleza kuwa hana mamlaka ya kuteua mrithi wa kakake mdogo, Raila.

“Kile nilifanya ni kumhimiza Wandayi atie bidii wala sikumteua kuwa mrithi. Nilisema kuwa anaendelea vizuri na ni miongoni mwa wandani wa Raila ambao nyota yao ya kisiasa huenda ikang’aa siku za usoni,” akawaambia wanahabari mjini Kisumu.

Seneta huyo wa Siaya alieleza kuwa hakuna pengo la uongozi eneo la Nyanza ambalo linapasa kutajwa, akiongeza kuwa Bw Odinga bado yu usukani na anaendelea vizuri.

Alimtaja kiongozi huyo wa Azimio kama mwanasiasa shupavu ambayo anajua kucheza karata zake vizuri zaidi.

Dkt Oginga alimtaka Bw Odinga kama mwanasiasa aliyejikuza kivyake, bila kusubiri kuidhinishwa na mtu yeyote kutoka jamii yake.

  • Tags

You can share this post!

Ndoa zasimama talaka zikipungua nchini, afichua Kadhi Mkuu

El Nino itasababisha njaa kubwa, walia wakazi wa Maya

T L