• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Ruto afukuza waandishi habari kwenye mkutano wake alioandaa Nakuru

Ruto afukuza waandishi habari kwenye mkutano wake alioandaa Nakuru

NA ERIC MATARA

NAIBU Rais William Ruto jana aliwazuia wanahabari kuangazia mkutano wa kisiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza alioongoza katika shamba la Hugo, eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru.

Dkt Ruto aliwaagiza walinzi wake kuwafurusha wanahabari waliokuwa wamefika katika mkutano huo, akishikilia kuwa lengo lake lilikuwa kujadili maslahi ya wenyeji, badala ya masuala ya kisiasa.

Dkt Ruto alikuwa akiendelea na hotuba yake alipotoa agizo hilo, akisema kikao hicho kilikuwa kikilenga kujadili masuala muhimu.

“Mbona wanahabari hawa wako hapa? Ni nani aliwaleta hapa? Tokeni kwanza ndipo tuzungumze mambo ya maana. Siwataki hapa,” akaagiza Dkt Ruto.

Wanahabari kutoka mashirika tofauti walilazimika kuondoka eneo hilo na kukaa kwa zaidi ya saa tatu wakingoja kuelezwa kuhusu yaliyojiri kwenye kikao hicho.

Baada ya Dkt Ruto na washirika wake kutoka kwenye kikao hicho, waliwahutubia wanahabari, wakisema kuwa walikuwa wakijadili masuala ya amani.

“Nilikuja hapa kuwahakikishia wenyeji wa Njoro na Molo kwamba mrengo wa Kenya Kwanza umejitolea kuhakikisha kuna amani na umoja uchaguzi mkuu wa Agosti unapokaribia. Washindani wangu wamekuwa wakieneza chuki kwenye kampeni zao. Hivyo, nilifika kuwarai wenyeji wa Njoro na Molo kudumisha amani, ikizingatiwa maeneo hayo yana wakazi kutoka jamii tofauti,” akasema Dkt Ruto.

“Ningetaka kuwahimiza washindani wangu pia kutoa hakikisho la kuzingatia amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu licha ya matokeo yatakavyokuwa,” akaeleza.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwepo kwenye kikao hicho walisema kuwa suala kuu lililojadiliwa ni kupungua kwa umaarufu wa muungano huo katika baadhi ya sehemu za Njoro na Molo.

Awali, Dkt Ruto alifanya kikao na Chama cha Watengenezaji Bidhaa Kenya (KAM) katika makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi.

Alikuwa ameandamana na mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua, Seneta Susan Kihika wa Nakuru kati ya viongozi wengine.

Mrengo wa Dkt Ruto umekuwa ukidai kuonewa na baadhi ya vyombo vya habari wanavyosema vinatumiwa kupigia debe wapinzani wao wa muungano wa Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Karua sasa ajitenga na Uhuru

Wazee kuamua rais wa tano wa Kenya

T L