• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Karua sasa ajitenga na Uhuru

Karua sasa ajitenga na Uhuru

NA WANDERI KAMAU

MGOMBEA-mwenza wa mwaniaji urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga, Bi Martha Karua, Jumatatu alionekana kujitenga na utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, kwenye hatua inayofasiriwa kama njia ya kutojihusisha na ‘dhambi’ za serikali ya Jubilee.

Kwenye mahojiano ya pamoja na vituo vya redio na televisheni vinavyotangaza katika eneo la Mlima Kenya, Bi Karua alisisitiza kuwa licha yake kuwa na uhusiano wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta, serikali iliyopo ni ya Chama cha Jubilee, wala si ya muungano wa Azimio.

“Serikali iliyo mamlakani kwa sasa ni ya Rais Uhuru Kenyatta na chama cha Jubilee. Viongozi wa muungano wa Azimio ni marafiki wa Rais Kenyatta. Hata hivyo, Azimio haipo serikalini. Jubilee iliyo serikalini ni sehemu ya muungano wa Azimio,” akasema Bi Karua.

Kauli hiyo inajiri siku moja tu baada ya Rais Kenyatta, Bi Karua na Bw Odinga kuhudhuria hafla ya pamoja katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi, Jumapili, ambapo wafuasi wa dhehebu la Akorino walikuwa wakiadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa dhehebu hilo nchini.

Katika hafla hiyo, Rais Kenyatta aliwaalika Bi Karua na Bw Odinga kuhutubu, ambapo waliupigia debe muungano wa Azimio.

Ijapokuwa Rais Kenyatta ameonyesha wazi kumuunga mkono Bw Odinga na Bi Karua kuwa warithi wake, hajakuwa akijitokeza kwenye mikutano yao ya kampeni.

Mnamo Jumatatu, Bi Karua alisema kuwa ingawa kuna baadhi ya mambo yanayoendeshwa na serikali ya Jubilee yatakayofanana na yale watakayoendesha na Bw Odinga ikiwa wataibuka washindi Agosti, kuna tofauti kubwa hata kwenye ahadi wanazotoa kwa Wakenya.

“Tofauti hizo huwepo katika mkondo wa siasa. Kwa wakati mmoja, Rais Kenyatta alihudumu kama Naibu Waziri Mkuu katika serikali ya hayati Mwai Kibaki. Lakini ukiangalia kwa kina, hata ikiwa kuna baadhi ya mambo yanayofanana katika serikali hizo mbili, bado kuna tofauti kubwa. Vivyo hivyo, ndivyo hali itakavyokuwa baada yetu kuibuka washindi. Hivyo, ningependa wafuasi wetu watofautishe urafiki na watu kushirikishwa kwenye serikali iliyopo,” akasema Bi Karua.

Akaongeza: “Kuna mambo tunayoweza kuwauliza marafiki wetu walio serikalini kutimiza. Kwa mfano, kuna baadhi ya mambo ambayo kiongozi wangu (Raila) anaahidi kuwatekelezea Wakenya. Hata hivyo, huwa anairai serikali kuyafanya, ingawa yeye hana nguvu wala mamlaka kuyatimiza kwa sababu hayuko serikalini.”

Serikali ya Rais Kenyatta imekuwa ikilaumiwa pakubwa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, bei za bidhaa za msingi na deni la kitaifa.

Wakati huo huo, Bi Karua alisisitiza kuwa jukumu lake kuu kama Naibu Rais na Waziri wa Haki na Masuala ya Kikatiba, litakuwa ni kuhakikisha ufisadi umekabiliwa kote serikalini.

Alitaja ufisadi kuwa “adui mkuu” wa ustawi katika nyanja zote.Alieleza kuwa lengo lake kuu litakuwa kuhakikisha wafisadi wote wanakabiliwa vikali kulingana na sheria, wala hawatalipiza kisasi.

“Ufisadi ndilo gonjwa kuu linalotuathiri katika serikali ya kitaifa na kaunti. Mipango mingi ya maendeleo imekwama kutokana na kuporwa kwa fedha za umma. Kama waziri atakayesimamia uendeshaji wa masuala ya haki, tutafuata sheria bila kulipiza kisasi dhidi ya yeyote na kuadhibu wafisadi,” akaeleza.

Kama njia ya kuhakikisha kuwa kesi za kawaida na zile zinazohusu ufisadi hazijikokoti mahakamani, Bi Karua aliahidi kubuni Sheria ya Kuharakisha Kesi zinaendeshwa na kumalizwa kwa haraka.

Bi Karua pia alimtetea vikali Bw Odinga, dhidi ya dhana kuwa yeye si maarufu katika eneo la Mlima Kenya.

Badala yake, alimsifia kuwa kiongozi shupavu na asiyejipenda, akitaja mchango wake kuwa uliomsaidia Bw Kibaki kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa 2002.

“Raila ndiye aliyemfanyia kampeni Bw Kibaki baada yake kuhusika kwenye ajali ya barabarani 2002. Amefungwa gerezani kwa miaka mingi akipigania ukombozi wa kisiasa nchini. Amekuwa akikosolewa na wapinzani wake kwa kuitwa kila jina bila kuwajibu. Sikitiko kuu ni kuwa baadhi ya wale wanaomkosoa ni wanafunzi wake kisiasa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ripoti ya Nyakango yaanika wazi kaunti...

Ruto afukuza waandishi habari kwenye mkutano wake alioandaa...

T L