• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Wazee kuamua rais wa tano wa Kenya

Wazee kuamua rais wa tano wa Kenya

NA LEONARD ONYANGO

WAPIGAKURA wa umri wa miaka 35 na zaidi ndio wataamua mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Hii ni kutokana na kuwa licha ya vijana kuwa ndio wengi, idadi ya waliojisajili kupiga kura ni ndogo kuliko ya wazee, hivyo kuwakosesha uamuzi mkubwa wa mshindi wa urais.Jumla ya wapigakura milioni 22 wamesajiliwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu, likiwa ni ongezeko la asilimia 12.8 ikilinganishwa na wapigakura milioni 19 mnamo 2017.

Kulingana na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, wapigakura milioni 13.3 ni wa kuanzia umri wa miaka 35 na zaidi huku vijana wa chini ya umri wa miaka 34 wakiwa milioni 8.8.

Wawaniaji wa urais wamekuwa wakilenga vijana katika kampeni zao kutokana na imani kwamba ndio wengi, lakini takwimu zilizotolewa jana zinaonyesha kuwa idadi ya vijana watakaoshiriki waliosajiliwa imepungua kwa asilimia 7.8 ikilinganishwa na 2017.

Watu milioni 7, wengi wao wakiwa vijana walio na vitambulisho vya kitaifa, walikosa kujisajili kuwa wapigakura, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa sajili ya wapigakura uliofanywa na kampuni ya KPMG.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa wanawake ni asilimia 49.12 ya wapigakura huku wanaume wakiwa 50.88.

Idadi ya vituo vitakavyotumika kupigia kura nayo imeongezeka kutoka elfu 40 mnamo 2017 hadi elfu 46. Hiyo inamaanisha kuwa kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wastani wa wapigakura 479.

Sheria ya uchaguzi inahitaji idadi ya wapigakura isipite watu 700 kwa kila kituo.IEBC imeondoa wapigakura wafu 246,465 kwenye sajili yake wengi wakiwa ni waliokufa.

Mkurugenzi Mtendaji wa IEBC, Marjan Hussein Marjan alisema kuwa tume hiyo itakabidhi kwa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) majina 4,757 ya watu ambao walijisajili zaidi ya mara moja kwa kutumia kitambulisho cha kitaifa na paspoti.

IEBC pia ilisema haitaondoa kwenye sajili majina ya watu elfu 164 waliosajiliwa lakini nambari zao za vitambulisho au paspoti zilikuwa na makosa pamoja na wengine elfu 481 waliosajiliwa bila kuweka nambari zao za vitambulisho au paspoti.

“Tunahofia kwamba tukiwaondoa huenda tukasababisha mpigakura halali akakosa kutekeleza haki yake ya kidemokrasia kuchagua viongozi anaowataka. Alama za vidole ndizo zitatumika kutambua wapigakura hivyo wapigakura feki hawatashiriki na halali wataruhusiwa kupiga kura licha ya maelezo yao yaliyomo katika sajili ya wapigakura kuwa na dosari,” akasema Bw Marjan.

Idadi ya wakenya wanaoishi ng’ambo watakaoshiriki uchaguzi wa mwaka huu imeongezeka hadi elfu 10 kutoka 4,223 mnamo 2017.

Idadi ya wafungwa watakaopiga kura pia imeongezeka hadi 7,483 kutoka 5,182 miaka mitano iliyopita.

Takwimu za IEBC pia zinaonyesha kuwa walemavu waliosajiliwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu ni milioni 4.2. Hii inamaanisha kuwa walemavu watakuwa na usemi mkubwa katika kuamua rais wa tano wa Kenya.

Bw Chebukati alikiri kuwa baadhi ya wapigakura walihamishwa kiholela bila idhini yao: “Ukaguzi wa KPMG uligundua kuwa watu kadhaa katika maeneobunge mbalimbali walihamishwa kiholela bila idhini yao. Lakini tayari tumerekebisha hitilafu hiyo.”

Mkuu huyo wa IEBC alisema kuwa sajili ya wapigakura itapelekwa katika vituo vyote vya kupigia kura kote nchini kuanzia Agosti 2 kuwezesha watu kuthibitisha majina yao.

IEBC inatarajiwa kupeleka ripoti ya ukaguzi huo katika Bunge la Kitaifa na Seneti, kwa mujibu wa matakwa ya sheria.

  • Tags

You can share this post!

Ruto afukuza waandishi habari kwenye mkutano wake alioandaa...

Maeneobunge 5 yaliyo na kura nyingi sasa kivutio kwa...

T L