• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Ruto atoa ahadi mpya kwa Wapwani huku wakazi wakimtajia mahangaiko yao

Ruto atoa ahadi mpya kwa Wapwani huku wakazi wakimtajia mahangaiko yao

NA WINNIE ATIENO NA MKAMBURI MWAWASI

VIONGOZI kutoka Pwani wametoa matakwa yao kwa Rais William Ruto ikiwemo hali duni ya elimu, dhuluma za kihistoria za mashamba na kukosekana kwa hospitali kuu ya kitaifa, ambayo inawalazimu wakazi kusafiri hadi hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta kupata matibabu.

Rais Ruto alifanya mkutano na Gavana kutoka kaunti zote sita wakiongozwa na Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Fatuma Achani (Kwale), Andrew Mwadime (Taita Taveta), Dado Godhana (Tana River) na Issa Timamy (Lamu) ili kujadili maendeleo ya Pwani.

“Nitaenda kutafuta kati ya Sh5 bilioni hadi Sh10 ili kuboresha hospitali zilizoko Pwani ili wakazi watibiwe humu humu badala ya kusafiri hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu,” alisema Rais Ruto.

Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani ndiyo kituo kikubwa zaidi cha afya katika ukanda huu kinachohudumia ukanda mzima.

Hata hivyo, hospitali hiyo ya vitanda 700 imekumbwa na changamoto hasa ukosefu wa dawa za kutosha na uhaba wa madaktari na wahudumu wa afya.

“Tulifanya mazungumzo ya wazi kwa masaa matatu, na kukiri kuwa kuna changamoto katika sekta ya elimu katika ukanda huu. Lakini tumekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua vikwazo hivyo. Tulikuwa tumetoa nafasi ya kuajiri walimu 5000 kutoka ukanda huu lakini bado kuna uhaba wa walimu 300,” alisema Rais Ruto.

Hata hivyo, Rais Ruto alisema eneo la Pwani bado halijajaza idadi hiyo kwa sababu ya uhaba wa walimu Pwani.

Alisema kuna pengo la walimu 350 akiwasihi viongozi kuhakikisha wanafunzi wanasomea taaluma hiyo.

“Tunajenga taasisi ya elimu ya juu eneo la Matuga kwa ajili ya mafunzo ya sekta ya uchumi wa baharini. Tumetenga Sh1 bilioni kwa ajili ya mradi huo. Nimemwomba Waziri wa Uchumi wa Bahari na Madini Bw Salim Mvurya kusimamia mradi hadi kukamilika kwake,” aliongeza Rais.

Alisema serikali yake inataka kuwapa ujuzi vijana wa Pwani ili kufungua uwezo wa uchumi wa baharini.

“Tunahitaji mafunzo sahihi, ujuzi na mtaji wa watu. Kwa sasa, tunapata shilingi 20 bilioni kutoka kwa bahari yetu lakini uwezo wake ni kati ya Sh120 bilioni na Sh150 bilioni kila mwaka,” alisema.

Rais alisema Kenya bado haijafungua uwezo wake wa Uchumi wa Baharini kutokana na ukosefu wa wataalam wanaohitajika.

Kuhusu maswala ya unyakuzi wa ardhi, Rais alikariri kuwa ana mpango wa kusuluhisha suala hilo kupitia mazungumzo na wamiliki wa ardhi ambao hawapo.

Utawala wake umetenga Sh1 bilioni kununua ardhi kutoka kwa wamiliki wa ardhi ambao hawapo ili kuwapa makazi maskwota.

Alisema wapima ardhi watasaidia katika kutatua mizengwe na wavamizi waliopewa hati miliki.

“Mimi natoa ahadi mwenyewe nina kila mpango na nia ya kutekeleza. Lazima tukomeshe changamoto za maskwota Pwani,” aliongeza Rais Ruto.

Rais Ruto alisema utawala wake utajenga nyumba za bei nafuu na soko katika ardhi ya VOK huko Nyali.

  • Tags

You can share this post!

DONDOO: Ndoa yadumu wiki 2 tu demu akidai jembe la mume ni...

Ole wako wewe mwenye kutumia simu msalani!

T L