• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Safaricom yaponea katika kesi ya Sh305 bilioni walalamishi wakizembea

Safaricom yaponea katika kesi ya Sh305 bilioni walalamishi wakizembea

NA RICHARD MUNGUTI

KAMPUNI za Safaricom na Vodafone zimepata ushindi mkubwa katika kesi ya Sh305 bilioni kuhusu shughuli za kutuma pesa katika mtandao wa M-Pesa.

Akizamisha kesi hiyo dhidi ya Safaricom na Vodafone, Jaji Nixon Sifuna alisema walalamishi watatu waliowasilisha kesi hiyo walikaidi maagizo ya mahakama ya kutakiwa kuwakabidhi washtakiwa 21 nakala za kesi hiyo.

Vodafone iliyo na makao yake makuu nchini Uingereza, ilishtakiwa pamoja na Safaricom kwa kuendeleza huduma za benki kupitia mtandao wa M-Pesa bila kudhibitiwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Walalamishi watatu – Gichuki Waigwa, Lucy Nzola na Godfrey Okutoyi waliomba mahakama kuu iamuru Vodafone iwafidie kwa Sh305 bilioni kwa kuendesha biashara ya benki kinyume cha sheria.

Akitupilia mbali kesi hiyo Jaji Sifuna alisema walalamishi walipuuza sheria na maagizo ya korti, aliyotoa Oktoba 4, 2023.

Katika uamuzi huo, Jaji Sifuna alisema aliwataka walalamishi hao watatu wawakabidhi washtakiwa 21 nakala za kesi dhidi yao wajue namna ya kujitetea lakini wakakaidi agizo hilo.

Jaji Sifuna alisema kwa vile walalamishi walikataa kutii na kutekeleza maagizo yake, kesi hiyo “imezama.”

Katika maagizo hayo, Jaji Sifuna alikuwa amesema, “Endapo walalamishi hawatafuata maagizo yangu kesi hii itakoma na kufutiliwa mbali.”

Jaji huyo alisababisha kicheko alipotoa mfano wa wanaofunga ndoa wanapouliza “ndoa iko ama haipo?”

Kuhusu kesi hiyo alisema “kesi hii ilikoma na haipo tena kwa vile maagizo ya Oktoba 4, 2023, hayakutekelezwa.”

Jaji huyo alisema “mahakama haitoi maagizo yasiyo na nguvu”.

“Maagizo yalikuwa endapo walalamishi hawatakuwa wameyatii katika muda wa siku 21 basi itayeyuka na kukoma kabisa. Hakutakuwa na kesi kamwe,” akasema.

Mawakili Njoroge Regeru na Kioko Kilukumi waliomba Jaji Sifuna atupilie mbali kesi hiyo kwa sababu ya utovu wa walalamishi.

“Hakuna kesi hapa mbele ya korti. Kesi hii ilizama pale siku 21 zilipotamatika,” Mabw Regeru na Kilukumi walisema.

Mawakili hao waliomba korti itupilie mbali kesi hiyo.

Lakini wakili Wilfred Nderitu aliomba msamaha akisema “washtakiwa waliwasilisha kesi tano mpya na ndizo alikuwa anazishughulikia.”

Bw Nderitu alisema baadhi ya kesi hizo zilikuwa zimeorodheshwa kusikilizwa Novemba 8, 2023.

Pia aliomba mahakama imruhusu awasilishe ushahidi katika kesi hiyo katika siku 14.

Akitoa uamuzi Jaji Sifuna alisema: “Kwa vile walalamishi walikaidi maagizo yangu kwamba wawasilishe ushahidi katika muda wa siku 21 kuanzia Oktoba 4, 2023, kesi hii imetupiliwa mbali.”

Pia alisema kesi zilizoshtakiwa na Safaricom na Vodafone zikiomba kesi ipelekwe kwa mpatanishi “sawia zimekufa pamoja na hii ya walalamishi watatu.”

Jaji huyo alisema walalamishi wako huru kushtaki upya.

  • Tags

You can share this post!

Sarah Kabu atumia Sh500,000 kuipa ngozi ulaini wa kipekee

Mkenya alaani hatua ya KRA kumpokonya marashi katika uwanja...

T L