• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Seneta amwambia Kawira ahakikishe bajeti inafikia idara zote

Seneta amwambia Kawira ahakikishe bajeti inafikia idara zote

NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Meru Kathuri Murungi amemtaka Gavana wa Kaunti hiyo Kawira Mwangaza kuhakikisha kuwa serikali yake inatumia pesa zilizotengewa Idara zote katika bajeti yake ya mwaka huu wa kifedha.

Bw Murungi ambaye pia ni Naibu Spika wa Seneti alisikitika kuwa kaunti hiyo ilitumia asilimia 61.96 pekee ya bajeti yake ya Sh12.6 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023, kulingana na ripoti ya Msimamizi wa Bajeti (CoB) iliyotolewa mwezi Julai.

Hii, kulingana na seneta huyo, inaashiria kuwa karibu asilimia 38 ya bajeti hiyo, sawa na Sh1.45 bilioni zilisalia katika Hazina ya Kitaifa, kwani hazikutumika.

“Inaudhi kuwa pesa kiasi kikubwa na ambazo zilitarajiwa kutumiwa kufaidi wakazi wa Meru, zilisalia katika Hazina ya Kitaifa kufikia mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, ilhali watu wetu wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi,” Bw Murungi akawaambia wanahabari mnamo Julai 31, 2023 afisini mwake katika Majengo ya Bunge, Nairobi.

Seneta huyo ambaye anahudumu muhula wa kwanza, alisema Idara ambazo hazikutumia kiasi kikubwa cha bajeti zao ni Idara ya Utumishi wa Umma, Idara ya Masuala ya Vijana na Michezo, Idara ya Afya na Idara ya Elimu.

“Kwa mfano, kati ya Sh384 milioni zilizotengewa Idara ya Utumishi wa Umma ni Sh344 milioni pekee zilizotumiwa. Aidha, kati ya Sh525 milioni zilizotengewa Idara ya Afya, ni Sh329 milioni pekee zilizotumika ilhali watu wetu wanahitaji dawa katika hospitali za umma,” Bw Murungi akasema.

Kati ya bajeti ya Sh12.6 bilioni ya kaunti ya Meru katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023, Sh8.9 bilioni zilitengewa matumizi ya kila siku huku Sh3.7 bilioni zikitengewa miradi ya maendeleo.

Aidha, fedha zilizotengewa kaunti hiyo kama ruzuku kwa ajili ya miradi mahsusi (conditional grants) zilikuwa Sh3.7 bilioni.

Bw Murungi pia alimtaka Gavana Mwangaza kuhakikisha kuwa fedha za maendeleo zinasambazwa kwa usawa katika wadi zote katika maeneobunge yote tisa na wadi 45 katika kaunti ya Meru.

“Binafsi ninakariri kuwa nitaendelea kutekeleza wajibu wangu kama Seneta kufuatilia utendakazi wa serikali ya Kaunti ya Meru kuhakikisha kuwa watu waliotuchagua wanafaidi. Huu ndio wajibu wangu kulingana na kipengele cha 96 cha Katiba,” akasema Bw Murungi.

Bi Mwangaza alichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 baada ya kumbwaga Kiraitu Murungi.

Aliingia afisini rasmi mnamo Agosti 27, 2022 baada ya kulishwa kiapo.

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Awamu ya nne ya upasuaji wa maiti yakamilika

Ripoti yapendekeza CBC ifanyiwe mageuzi makuu

T L