• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Serikali kuhakikisha wakazi wa mitaa ya mabanda wanapata stima salama

Serikali kuhakikisha wakazi wa mitaa ya mabanda wanapata stima salama

Na SAMMY KIMATU

SERIKALI imepanga mikakati ya kuwapatia wananchi stima iliyo safi na salama.

Mkuu wa tarafa ya South B, Kaunti ya Nairobi Michael Aswani Were alisema nia ya mpango huo ni kumaliza uunganishaji wa stima kiholela tena kiharamu kwenye mitaa ya mabanda na kuepusha mauti.

Aidha, Bw Were aliongeza kwamba serikali imelenga kuokoa mamilioni ya pesa zinazopotea baada ya matapeli na mabroka kufisidi kampuni ya Kenya Power.

“Serikali inalenga kupatia wananchi stima iliyo safi na salama wanapoitumia nyumbani sawia na viwandani. Pia inanuia kumaliza visa vya vifo vinavyotokana na watu kuuawa na stima wakijiunganishia kiholela,” Bw Were akaambia Taifa Leo.

Ili kufanikisha mpango huo, Bw Were alisema maafisa wa Kenya Power watashirikiana na wakazi katika mitaa ya mabanda kupitia vikundi mbalimbali na viongozi wengine mitaani.

“Tutashirikiana na wakazi kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii pamoja na viongozi mbalimbali katika kila mtaa,” Bw Were akasema.

Kufuatia kuongezeka kwa visa vya transfoma kulipuka mara kwa mara, aliongeza kwamba kampuni hiyo imekadiria hasara kubwa kwani wakazi kwenye mitaa ya mabanda hawalipi stima ilhali wao huitumia.

“Kusema ukweli, wamiliki wa nyumba na wapangaji ndio huumia kwa kutozwa ada ya stima na watapeli na mabroka wa stima ilhali kampuni ya Kenya Power inakosa mapato,” akadokeza Bw Were.

Wiki jana, maafisa wa Kenya Power waliondoa na kubeba transfoma mkabala wa barabara ya Aoko karibu na kanisa la South B All Nations Pefa.

Kufutaia tukio hilo, mitaa miwili ya mabanda kwenye eneo la South B imegubikwa na giza totoro na kuathiri biashara za wakazi kwenye mitaa husika.

Mitaa hiyo ni Mukuru-Sokoni na Mukuru-Kisii Village.

Mwaka 2020 kampuni hiyo iliondoa transfoma katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Njenga, Lunga Lunga, Sinai, Paradise, Kwa Reuben, Kayaba, Hazina na nyingine mkabala wa barabara ya Enterprise.

Bw Were aliongeza kwamba serikali inataka taratibu zifaao kufuatwa kisheria kwa yeyote kupatiwa nguvu za umeme.

“Lazima sheria zifuatwe kwa mtu yeyote anayetaka kuunganishiwa stima kwa matumizi yake mitaani. Pia serikali haitaki kupoteza maisha ya watu wake kutokana na vifo bvinavyohusiana na nguvu za umeme katika mitaa yetu,” Bw Were akaonya.

Kadhalika, alisema kuanzia wiki hii, kutakuwa na msururu wa mikutano kati ya wakazi na maafisa wa Kenya Power na kuwaomba wakazi kushirikiana na maafisa hao.

  • Tags

You can share this post!

Peru yakomoa Venezuela na kuingia robo-fainali za Copa...

Vipusa wa Arsenal wapata kocha mpya