• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Serikali kuharibu sukari ya Sh1 bilioni kutoka Zimbabwe

Serikali kuharibu sukari ya Sh1 bilioni kutoka Zimbabwe

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imepanga kuharibu sukari ya thamani ya mamilioni ya fedha kutoka Zimbabwe ambayo imekuwa katika Bandari ya Mombasa tangu 2018.

Meneja Mkuu wa Bandari ya Mombasa Abdi Malik Hussein, kupitia notisi iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali, Ijumaa, alisema sukari hiyo ya uzani wa tani 20,000 itaharibiwa Agosti 3, 2021.

Sukari hiyo imehifadhiwa katika makontena 40 ya tani 500 kila moja na iliwasili katika Bandari ya Mombasa Julai 15, 2018 kupitia meli MSC Nicole, kulingana na Bw Hussein.

Sukari hiyo ilikuwa mali ya Sirocco Investments iliyo na afisi zake jijini Nairobi.

“Mnafahamishwa kuwa bidhaa hiyo ambayo imeharibika itaharibiwa siku 30 baada ya kutolewa kwa notisi hii,” akasema Bw Hussein.

Hata hivyo, haijulikani ni kwa nini kampuni ya Sirocco Investments ilishindwa kuchukua shehena hiyo ya sukari.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ambapo sukari inauzwa kwa bei ghali.

Inakadiriwa kuwa tani moja ya sukari inagharimu Sh80,000 humu nchini ikilinganishwa na mataifa mengine ambapo kiasi sawa huuzwa kwa hadi Sh28,000.

Hiyo inamaanisha kuwa kampuni ya Sirocco Investments imepoteza zaidi ya Sh1 bilioni.

Kufikia 2018, kulikuwa na kampuni 60 ambazo zimeidhinishwa kuagiza sukari kutoka nje.

Kenya inakabiliwa na uhaba wa sukari wa tani 600,000 kila mwaka na pengo hilo hujazwa na wafanyabiashara hao ambao wanaagiza bidhaa hiyo kutoka ughaibuni.

Mnamo 2019, sukari iliyoshukiwa kuwa na sumu ilitoweka katika hali ya kutatanisha kutoka maghala ya Changamwe na Jomvu Kaunti ya Mombasa ilipokuwa imehifadhiwa.

Sukari hiyo iliyonaswa na Mamlaka ya Ushuru (KRA) na Shirika la Kuhakiki Ubora wa Bidhaa (Kebs) ilidaiwa kuwa na madini ya mekyuri na kopa ambayo ni hatari kwa afya kwani yanasababisha kansa.

You can share this post!

Wakazi wa Gatukuyu kupata soko jipya

Fulham wamwajiri kocha Marco Silva kuwa mrithi wa Scott...