• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Wakazi wa Gatukuyu kupata soko jipya

Wakazi wa Gatukuyu kupata soko jipya

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Gatukuyu lililoko Gatundu Kaskazini, watanufaika kutokana na mradi wa ujenzi wa soko jipya.

Kulingana na Gavana wa Kaunti ya Kiambu, Dkt James Nyoro, tayari kaunti hiyo imetenga takribani Sh800 milioni kukamilisha ujenzi wa masoko saba.

“Kaunti ya Kiambu itafanya juhudi kuona ya kwamba soko hilo linakamilika jinsi ilivyopangwa. Ninawasihi nyinyi wakazi wa eneo hili mshirikiane na wajenzi wa soko hili ili kuwe na uhusiano mwema,” Dkt Nyoro aliwashauri wakazi wa Gatukuyu.

Alisema miradi yote inayoendelea kwa sasa ni sharti ikamilishwe ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao wa 2022.

Mfanyabiashara katika soko la Gatukuyu Bi Mary Njeri Waweru alikiri wamekuwa na shida kwa zaidi ya miaka 20.

“Sisi kama wenyeji wa hapa tumepitia matatizo mengi hasa wakati wa mvua kutokana na matope na kukosa vyoo vya kwenda haja,” alifafanua Bi Waweru.

Wakazi hao wanasema wakati soko hilo litakamilika, bila shaka utakuwa ni mwamko mpya wa kibiashara.

Soko hilo litakuwa na uwezo wa kubeba watu 800 kwa wakati mmoja, ambapo kila mmoja atapewa mahali pake pa kuuzia bidhaa zake.

Wakazi hao pia wametaka wajenzi wa mradi huo wa soko wafanye juhudi kuona ya kwamba vijana wa eneo hilo wamepata vibarua ili wapate mkate wa kila siku.

Pendekezo hilo lilikubaliwa na gavana mwenyewe aliyesema atafuatilia jambo hilo kuona ya kwamba vijana hao wananufaika moja kwa moja na ujenzi huo.

Kulingana na mpangilio wa Kaunti ya Kiambu, soko hilo linajengwa kwa muundo wa kisasa ambapo umeme, maji, vyoo, na ulinzi wa kutosha ni mambo muhimu yatakayozingatiwa.

Baadhi ya masoko yaliyokamilika ni ya Kikuyu, Githurai, na Ruiru huku yale ya Makongeni, Thika na Wangige yakikaribia kukamilika.

Baada ya soko hilo kukamilika litanufaisha pakubwa wakazi wa kutoka Makwa, Mang’u, Kamwangi na hata Thika.

You can share this post!

Gilmour atua Norwich kwa mkopo, Juan Mata asalia Manchester...

Serikali kuharibu sukari ya Sh1 bilioni kutoka Zimbabwe