• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Fulham wamwajiri kocha Marco Silva kuwa mrithi wa Scott Parker aliyeyoyomea Bournemouth

Fulham wamwajiri kocha Marco Silva kuwa mrithi wa Scott Parker aliyeyoyomea Bournemouth

Na MASHIRIKA

FULHAM wamemteua Marco Silva ambaye ni mkufunzi wa zamani wa Everton na Watford kuwa kocha wao kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kocha huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 43 anamrithi Scott Parker aliyeondoka uwanjani Craven Cottage mnamo Juni 28 na kuyoyomea ugani Vitality kudhibiti mikoba ya Bournemouth ambao pia wanashiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Nyota wa zamani wa Fulham, Luis Boa Morte amerejea kambini mwa Fulham kuwa kocha msaidizi.

Silba alianza kunogesha soka ya Uingereza akiwa kocha wa Hull City mnamo 2017. Awali, alikuwa amedhibiti mikoba ya Sporting Lisbon na Olympiakos nchini Ureno na Ugiriki mtawalia.

“Nina furaha kubwa. Naona fahari na tija kuteuliwa kuwa kocha wa kikosi hiki kinachojivunia historia pana katika ulingo wa soka,” akasema Silva aliyeanza kazi ya ukocha akiwatia makali vijana wa kikosi cha Estoril FC nchini Ureno.

Silva hajawahi kunoa kikosi kinachoshiriki kipute cha Championship, ingawa Hull City waliwahi kushushwa ngazi kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi kivumbi hicho katika kipindi cha miezi mitano aliyodhibiti mikoba ya klabu hiyo mnamo 2017.

Aliaminiwa kuwa mrithi wa Mike Phelan mnamo Januari 2017 Hull walipokuwa mkiani mwa jedwali la EPL. Japo mchango wake ulinyanyua kikosi hadi nafasi ya tatu kutoka mwisho, hakufaulu kuzuia klabu hiyo kuteremshwa ngazi.

Silva alihamia Watfod baadaye na akaongoza kikosi hicho kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya 17 jedwalini. Hata hivyo, alipigwa kalamu mnao Januari 2018 baada ya kuanza kuhusishwa na Everton.

Katika msimu wake wa kwanza ugani Goodison Park, aliongoza Everton kukamilisha kipute cha EPL katika nafasi ya nane ligini japo akatimuliwa mwishoni mwa 2019 baada ya waajiri wake kupepetwa 5-2 na mahasimu wa tangu jadi, Liverpool.

Katika enzi yake ya usogora, Boa Morte aliwajibishwa na Fulham mara 250 chini ya kipindi cha miaka sita na nusu aliyohudumu ugani Craven Cottage.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Serikali kuharibu sukari ya Sh1 bilioni kutoka Zimbabwe

Polisi wawili wafyatuliana risasi wakizozania mwanadada