• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Serikali yahimizwa kutilia mkazo miradi ya uongezaji thamani kwa bidhaa za mazao ya kilimo 

Serikali yahimizwa kutilia mkazo miradi ya uongezaji thamani kwa bidhaa za mazao ya kilimo 

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imehimizwa kutilia maanani suala la uongezaji thamani mazao mabichi ya kilimo, ili kuepuka uharibifu wa mazao shambani.

Balozi wa Uholanzi nchini Kenya, Marteen Brouwer ameishauri serikali kutathmini na kutilia mkazo miradi ya uongezaji thamani.

Brouwer amesema changamoto zinazozingira wakulima nchini, hasa mazao kuozea shambani na pia sokoni kwa sababu ya ukosefu wa soko, zitaangaziwa kupitia uongezaji thamani.

“Kimsingi, maendeleo ya taifa, ikizingatiwa kuwa kilimo ni mojawapo ya nguzo kuu za Kenya, yatashuhudiwa kupitia uanzishaji miradi na viwanda vya kutengeza bidhaa zitokanazo na mazao ya shambani,” balozi huyo akasema.

Balozi wa Uholanzi nchini Kenya, Marteen Brouwer akitangamana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni moja ya kuongeza thamani mazao ya kilimo jijini Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Akaongeza: “Serikali ni kiungo muhimu katika uboreshaji wa taifa na maendeleo, na itakuwa jambo la busara ikiwa itafanikisha miundomsingi inayohitajitaka katika viwanda vya kuongeza mazao thamani.”

Akiipongeza serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu Ajenda Nne Kuu ikiwemo ustawi wa viwanda, balozi huyo amehimiza haja ya sekta hiyo, hususan ya vyakula kupigwa jeki kwa hali na mali.

“Viwanda vingi vya chakula vikizinduliwa na vilivyopo kuinuliwa, kero ya mazao ya kilimo kuoza itakuwa historia. Kuna watu wengi sana wanahitaji lishe, wakati ambapo bidhaa zinaharibika,” akasema.

Uholanzi ni taifa la pili bora duniani kuimarisha sekta ya viwanda vya bidhaa za kula, serikali ya nchi hiyo ikipiga jeki wakulima kwa hali na mali.

Aidha, nchi hiyo pia ni tajika katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ikiwa ni pamoja na kukumbatia teknolojia ya kisasa kuendeleza ufugaji na kilimo.

Balozi amesema hayo katika hafla moja jijini Nairobi, iliyoleta pamoja kampuni kadha zinazotoa huduma za kilimo nchini, ambapo aliahidi kwamba Uholanzi itajituma kuinua mashirika na kampuni hizo.

 

You can share this post!

NDONDI: Timu ya taifa yaimarisha maandalizi ya Olimpiki

Gilmour atua Norwich kwa mkopo, Juan Mata asalia Manchester...