• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
NDONDI: Timu ya taifa yaimarisha maandalizi ya Olimpiki

NDONDI: Timu ya taifa yaimarisha maandalizi ya Olimpiki

Na CHARLES ONGADI

TIMU ya taifa ya ndondi imeimarisha maandalizi yake kwa michezo ya Olimpiki huku ikisalia na wiki mbili kuondoka nchini kueleka Tokyo, Japan.

Kikosi cha mabondia 12 na wakufunzi 5, ilihamisha kambi yake ya mazoezi kutoka ukumbi wa AV Fitness, Lavington hadi uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani (MISC) wiki mbili zilizopita.

Wakati huo huo, Shirikisho la Ndondi Nchini (BFK) imeimarisha benchi la ufundi ya ‘Hit Squad’ ikijumuisha wakufunzi wawili wenye tajriba katika mchezo huu.

Mshindi wa nishani ya shaba katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 1984 iliyoandaliwa Los Angeles, Amerika, Ibrahim ‘Surf’ Bilali na kocha wa klabu ya Dallas ya Muthurwa, Charles Mukula wamejumuishwa kikosini.

Aidha, kocha mkuu Musa Benjamin amefichua kwamba wamekuwa wakijaribu kurekebisha kadri ya uwezo wao makosa yaliyojiri katika mashindano walioshiriki mara ya mwisho nchini Urusi.

“Tumekuwa tukirekebisha kasi na nguvu ya mabondia wetu katika mazoezi yetu na kumekuwa na mabadiliko makubwa,” akasema kocha Benjamin.

Kulingana na naibu kocha David Munuhe, hadi kufikia sasa mabondia wanne waliofuzu kushiriki michezo ya Olimpiki wako katika hali nzuri na tayari kupeperusha bendera ya taifa jijini Tokyo, Japan.

Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya mabondia hao, nahodha Nick ‘Commander ‘ Okoth amesema wanaenda nchini Japan kwa lengo la kurudi nyumbani na medali.

“Hakuna medali katika Olimpiki iliyowekewa bondia yeyote wala iliyo na jina kwa hivyo tunaenda nchini Japan kung’ang’ania medali hizo bila kuogopa kwa sababu tumejiandaa barabara, “ akasema Okoth.

Kwa mujibu wa kocha david Munuhe, kikosi ha ‘ Hit Squad ‘ inayojumuisha mabondia Christina Ongare (fly), nick ‘ Commander ‘ Okoth (unyoya), Elizabeth Akinyi (welter) na Elly Ajowi kinatarajiwa kuondoka nchini Julai kuelekea Tokyo, Japan.

Bondia wa kike Elizabeth Akinyi atakayeshiriki michezo ya Olimpiki katika kitengo cha uzani wa welter. Ana matumaini ya kufanya vyema katika mashindano haya atakayoshiriki kwa mara ya kwanza. Picha/ Charles Ongadi

Michezo ya Olympiki inatarajiwa kung’oa nanga Julai 23 hadi Agosti 9, 2021.

You can share this post!

Sergio Ramos akubali kuchezea PSG kwa mkataba wa miaka...

Serikali yahimizwa kutilia mkazo miradi ya uongezaji...