• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Serikali yawataka wazazi walinde watoto dhidi ya dhuluma na habari potovu mitandaoni

Serikali yawataka wazazi walinde watoto dhidi ya dhuluma na habari potovu mitandaoni

Na WINNIE ONYANDO

SERIKALI inawataka wazazi kuwajibika na kuwalinda watoto wao dhidi ya habari potovu na dhuluma mtandaoni.

Waziri wa Mawasiliano, Joe Mucheru aliwalaumu wazazi kwa kukosa kukagua wavuti wanazoingia watoto wao, jambo linalosababisha kuongezeka kwa visa vya dhuluma za watoto mitandaoni.

Akizungumza jana katika hafla ya uzinduzi wa programu ya kuwalinda watoto mitandaoni iliyoasisiwa na Mama wa Taifa, Bi Margaret Kenyatta jijini Nairobi, Bw Mucheru alisema kuweka nywila (pin) kwenye simu au kwenye wavuti mbalimbali hakutoshi.

“Hatuwezi kuwalaumu watoto wetu. Lawama ni kwa wazazi ambao mara nyingi huwa wazembe baada ya kuwapa watoto wao simu. Ni jukumu letu sote kupambana na dhuluma za watoto mitandaoni. Wazazi lazima wawe katika mstari wa mbele katika kutekeleza hilo,” akashauri Bw Mucheru.

Alihusisha mavazi mabaya, matumizi ya lugha chafu, mitindo inayokiuka tamaduni za Kiafrika na vifo miongoni mwa watoto na ukosefu wa wazazi kuweka mipaka katika habari wanazofaa kuzitazama watoto wao.

“Wewe kama mzazi, hufai kumwacha mtoto wako huru kuingia katika wavuti yoyote. Weka mipaka ya matumizi ya simu. Usimwache atumie simu kwa muda mrefu,” akaonya Bw Mucheru.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano, Mercy Wanja, alisema matumizi ya mtandao yaliongezeka kwa asilimia nne mwaka huu kutokana na janga la corona. Aliwataka wazazi wahakikishe kuwa watoto wanapata tu fursa ya kufikia wavuti zinazohusiana na elimu bali si za kuwapotosha.

“Uzinduzi wa kampeni hii ni njia ya kuwalinda watoto wetu. Hatutaki wafikie habari za kuwapotosha,” akasema Bi Wanja.

Hata hivyo, Bi Wanja alisema watashirikiana na walimu na Taasisi ya Mtaala (KICD) ili kuunda wavuti itakayoangazia masuala ya watoto na kuwapa mafunzo ya kiakademia.

Alisema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile Wizara ya Elimu, KICD, Ofisi ya wapelelezi wa makosa ya jinai na mahakama kuu ili kuwachukulia hatua watakaopatikana wakiwadhulumu watoto mtandaoni.

Jaji Mkuu, Martha Koome ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema tayari wameunda programu mtandaoni itakayotumika kurekodi kesi zote na kuwawezesha polisi kufuatilia kesi zote za dhuluma.

You can share this post!

Kalonzo awarai vinara wa OKA kumpa tiketi kuwania urais 2022

Kega: Seneta Moi ametosha unga kumrithi Rais Kenyatta