• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:52 PM
Shakahola: Idadi jumla ya watu waliothibitishwa kufariki ni 338

Shakahola: Idadi jumla ya watu waliothibitishwa kufariki ni 338

NA ALEX KALAMA

IDADI ya miili iliyofanyiwa upasuaji katika awamu ya tatu ya upasuaji wa maiti za wahanga wa imani potovu zilizofukuliwa kutoka eneo la Shakahola katika Kaunti ya Kilifi imefika 87 baada ya miili 22 zaidi kufanyiwa upasuaji mnamo Jumatatu.

Hata hivyo idadi ya miili iliyofukuliwa katika awamu ya tatu imeongezeka kutoka 94 hadi 96 baada ya miili miwili kutambulika kuwa ilihifadhiwa katika mfuko mmoja huku mtu mmoja zaidi kutoka eneo hilo akifariki akiwa kizuizini.

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor anasema kuwa asilimia kubwa ya miili iliyofanyiwa upasuaji ni ya watu waliofariki kutokana na ukosefu wa chakula.

Mwanapatholojia huyo amedokeza kuwa kati ya miili 22 iliyofanyiwa uchunguzi mnamo Jumatatu 14 ilikuwa ya watoto huku akiongeza kuwa kufikia sasa idadi kamili ya maiti za wahanga wa imani potovu imefikia 338 kutokana na miili miwili kugunduliwa ilikuwa imehifadhiwa katika mfuko mmoja huku mwili mwingine ukiwa ni ule wa mshukiwa aliyeaga dunia akiwa gerezani.

Vile vile Oduor amebainisha kuwa miili tisa iliyosalia itafanyiwa upasuaji hapo kesho Jumanne katika mochari ya Hospitali Kuu ya kaunti ndogo ya Malindi kabla ya kuanza kwa awamu ya nne ya ufukuaji wa makaburi kuondoa miili.

Aidha Bw Oduor ameeleza kuwa kwa baadhi ya miili hiyo, imekuwa vigumu wao kutambua kiini cha vifo vya watu hao kutokana na sababu kwamba miili hiyo ilikuwa imeharibika kupita kiasi.

  • Tags

You can share this post!

Rais atia saini Mswada wa Fedha wa 2023

Jopo la kuteua DPP mpya laapishwa kuanza kazi rasmi

T L