• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Simanzi wanafunzi 3, dereva wakifariki ajalini

Simanzi wanafunzi 3, dereva wakifariki ajalini

WANAFUNZI watatu wa shule ya Upili ya Wasichana ya Chogoria na dereva wa matatu walilokuwa wameabiri kuelekea Nairobi wamefariki katika ajali.

Wasichana wengine 10 wa shule hiyo walikimbizwa katika hospitali tofauti wakiwa na majeraha.

Gari hilo linalomilikiwa na chama cha Akiba na Mikopo cha matatu cha MAK One lilikuwa limebeba wanafunzi 14 ajali ilipotokea.

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi mwendo wa saa mbili asubuhi eneo la Area 49 kwenye barabara ya Sagana-Kenol na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Kulingana na kamanda wa polisi wa Murang’a Kusini, Alexander Shikondi, dereva huyo aliyefariki alifanya kosa la kutokuwa makini.

“Matatu iliyobeba wanafunzi hao ilikuwa ikielekea Nairobi. Mbele yake kulikuwa na trela na aliamua kuipita. Trela iligongana na matatu hilo, jambo lililosababisha ajali hiyo,” akasema Bw Shikondi.

Alithibitisha kuwa watu 10 waliojeruhiwa walikimbizwa hospitalini.

“Tunaendelea kufuatilia hali za walionusurika. Tunawasiliana na madaktari na pia tumewasiliana na usimamizi wa shule ili kutoa taarifa kwa wazazi wa wanafunzi hao,” akasema Bw Shikondi.

Mwanamke aliyeshuhudia ajali hiyo, Marian Nkunini, alisema mgongano wa magari hayo ulisababisha kelele na nduru kutoka kwa walioathiriwa.

Alisema kuwa alishtuliwa na ajali hiyo na kuwaita watu ili kuwaokoa waliothiriwa.

“Niliposhuhudia ajali hiyo, nilipiga magoti na kuomba Mungu awaokoe walioathiriwa. Nilishtuka kuwaona baadhi ya wanafunzi wakitolewa wakiwa wamekufa,” akasema Bi Nkunini.

Bw Shikondi alitoa wito kwa madereva kuwa waangalifu hasa msimu huu wa Krismasi.

“Baadhi ya ajali zinaweza kuepukika ikiwa tutafuata kanuni zote za trafiki. Madereva hawafai kuendesha magari kwa kasi na kusahau kuwa maisha ya abiria yako mikononi mwao. Ni wakati wa sherehe na likizo na ni vyema kila mmoja ajihadhari,” akaonya Bw Shikondi.

Wiki jana, wanafunzi watano wa shule walipata majeraha na dereva kupoteza maisha yake.

You can share this post!

Amri meli yenye vifaa hatari itengwe

Mwalimu aliyejichoma aaga dunia akitibiwa

T L