• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Sofapaka kukabili Ulinzi, Gor na AFC wakipambana na wapinzani kesho

Sofapaka kukabili Ulinzi, Gor na AFC wakipambana na wapinzani kesho

BAADA ya kuchapwa na Gor Mahia kwenye mechi iliyojaa utata mwingi wikendi iliyopita, mabingwa wa 2009 Sofapaka hii leo wana kibarua kigumu dhidi ya Ulinzi Stars katika kipute kikali cha Ligi Kuu ugani Utalii, Nairobi.

Mechi hiyo na nyingine tatu zimeratibiwa leo huku nyingine zaidi zikitarajiwa kusakatwa kesho wakati ambapo ushindani wa kuwania ubingwa unaendelea kushika kasi. Kando na Sofapaka na Ulinzi Stars, mechi nyingine inayotarajiwa kusisimua hii leo ni kati ya Bandari na Kariobangi Sharks ugani Mbaraki.

Mnamo Jumamosi, mabingwa watetezi Gor Mahia wataikaribisha Western Stima ugani Thika huku Wazito waliotoka sare tasa na K’Ogalo wakipepetana na mabingwa mara 13 AFC Leopards ugani Ruaraka.Mkufunzi wa Sofapaka Ken Odhiambo alieleza imani yake kwamba wataipiku Ulinzi Stars licha ya kuchapwa na Gor kwenye mechi yao iliyopita.

Ulinzi Stars ambao hawajapoteza katika mechi nne zilizopita ni wapinzani wakali na mechi hiyo inatarajiwa kusisimua mno kati ya pande zote mbili.“Sitaki kuzungumzia jinsi tulivyohujumiwa na Gor ila dhidi ya Ulinzi Stars ni lazima tushinde na kupata matokeo mema uwanjani.

Itakuwa mechi ngumu kwa pande zote lakini tunalenga ushindi ili kutoa ushindani mkali dhidi ya timu za juu katika msimamo wa jedwali,” Odhiambo akaeleza Taifa Leo.Huku ‘Batoto ba Mungu’ ikiwa katika nafasi ya 12 kwa alama 23 baada ya mechi 20, Ulinzi Stars wapo katika nafasi ya nane kwa alama 26 na ushindi huenda ukaivukisha hadi nafasi ya sita katika msimamo wa jedwali.

Hapo kesho, Gor na AFC Leopards ambazo zilijikwaa dhidi ya Wazito na wavuta mkia Mathare United wana kibarua kigumu, huku K’Ogalo wakiiandaa Western Stima nayo Leopards ikipambana na wenye ngwenje Wazito ugani Ruaraka.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wapewa tahadhari kuhusu mkurupuko wa nimonia

Kituo cha polisi chafungwa kutokana na corona