• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Wazazi wapewa tahadhari kuhusu mkurupuko wa nimonia

Wazazi wapewa tahadhari kuhusu mkurupuko wa nimonia

Na STEPHEN ODUOR

WAZAZI katika Kaunti ya Tana River wameonywa dhidi ya kupuuza dalili za homa kwa watoto kwa vile kuna mkurupuko wa nimonia.

Zaidi ya magonjwa 20 ya nimonia kwa watoto yameripotiwa katika Hospital Kuu mjini Hola, huku vifo vinne vikitokea chini ya miezi miwili kutokana na hali hiyo.Magonjwa mengine yanaendelea kuripotiwa katika hospitali na zahanati za nyanjani, ambapo zaidi ya watoto 30 wamelazwa kwa matibabu wakiwa katika hali mbaya.

Akizungumza na Taifa Leo mjini Hola, afisa anayesimamia afya ya watoto, Bw Joseph Ndegwa alisema kuwa baadhi ya wazazi walikuwa wakipuuza ugonjwa huo wakiudhani ni homa ya kawaida hadi pale afya ya watoto inapozorota.

“Wazazi wanawaleta watoto hospitalini wakiwa hali mahututi, wakati ambapo homa hiyo imedhuru sana mapafu ya watoto,” alisema.Bw Ndegwa alisema kuwa baadhi ya watoto hufikishwa hospitalini wakihitaji usaidizi wa kupumua na hivyo kuwagharimu wazazi hao zaidi kifedha.

Alisema kuwa hapakuwa na mitungi ya kutosha ya oksijeni na hivyo basi ilikuwa vigumu kuokoa baadhi ya maisha ya watoto hao.“Nimonia haifai kucheleweshwa kimatibabu. Mzazi yeyote anapoona dalili za homa ni vyema kufika hospitalini kwa uchunguzi zaidi,” akasema.

Zaidi ya hayo, Bw Ndegwa alisema baridi tele inayoshuhudiwa kwa sasa inafanya iwe rahisi kwa watoto kuathirika na homa hiyo.Aliwarai wazazi kuwavalisha wanao nguo za kuwapa joto na kuwaepusha na vinywaji baridi msimu huu.

Pia amewataka wazazi hao kutilia maanani ushauri wa madakitari hususan kwa kuzingatia utaratibu wa kumeza dawa.“Tumegundua kuwa wazazi wengi hawamalizi vipimo vya dawa, hivyo baada ya siku chache unapata mzazi amemrejesha mtoto akiwa katika hali mbaya zaidi,” akasema

  • Tags

You can share this post!

Lissu kuzindua kitabu chake leo Nairobi

Sofapaka kukabili Ulinzi, Gor na AFC wakipambana na...