• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Sonko awa mwiba kwa wanasiasa na maafisa serikalini

Sonko awa mwiba kwa wanasiasa na maafisa serikalini

Na BENSON MATHEKA

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi Mike Sonko amekuwa sumu kwa wanasiasa na maafisa wa serikali wanaohofia kuwa huenda alirekodi mazungumzo yao kisiri kwa nia ya kuyaanika jinsi amekuwa akifanya.

Wiki mbili zilizopita, Bw Sonko alitoa video alizohusisha Jaji Said Chitembwe na madai ya ufisadi.

Jaji huyo amekanusha madai ya Bw Sonko ambayo yanachunguzwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).

Bw Sonko anakiri kwamba amekuwa akirekodi mazungumzo na mikutano yake na viongozi na maafisa wakuu wa serikali na hatasita kuyaanika kufahamisha umma mienendo yao.

Baadhi yao, akiwemo Gavana wa Nairobi Ann Kananu wamepata agizo la mahakama kumzuia Bw Sonko kuchapisha habari zozote kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaweza kumpaka tope.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, Bw Sonko anatoa vitisho hivyo makusudi kwa kuwa uchaguzi mkuu unakaribia na wanasiasa wengi wanaazimia kugombea viti mbali mbali.

“Bw Sonko anajua anachofanya. Analenga wanasiasa na maafisa wa serikali kwa sababu uchaguzi mkuu unakaribia na anaweza kuwa sumu kwa wengi ikizingatiwa alipokuwa gavana, alikuwa akitembelewa na kukutana na wengi wao, baadhi ambao huenda walitaka wasaidiane kwa njia moja au nyingine viongozi wanavyofanya kila wakati,” asema mchaganuzi wa siasa Geff Kamwanah.

KISASI

Vile vile, anasema kwamba Bw Sonko anaonekana kuwa na kisasi na watu ambao walichangia kwa njia moja au nyingine masaibu yake ya kisiasa na hata kibiashara.

“Anaonekana kuwa na kisasi na baadhi ya watu hasa wale anaohisi walihusika na kutimuliwa kwake ofisini. Kwa sasa hakuna anayefahamu ataanika nani siku zijazo hasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” asema Bw Kamwanah.

Wachanganuzi wanasema wanaofaa kuingiwa na wasiwasi ni wale ambao wamewahi kutangamana naye kwa shughuli zisizo rasmi.

“Tabia ya Bw Sonko inaweza kuporomosha maisha ya kisiasa na kitaaluma ya watu wengi hasa walio katika utumishi wa umma na biashara ambazo zinahitaji kulindwa ili kudumisha imani ya wateja,” asema Bi Beth Wanjira, mtaalamu wa masuala maadili.

Anasema anachofanya Bw Sonko ni kubomoa imani ambayo watu walikuwa nayo kwake.

“Anatoa taswira ya mtu ambaye amekata tamaa, anayejitosheleza na ambaye hahitaji watu katika maisha na shughuli zake za kila siku. Watu watakuwa wakimuambaa,” asema.

Akihojiwa na runinga maarufu nchini wiki jana, Bw Sonko alisema kwamba alisema lengo lake la kurekodi mikutano na mawasiliano yake na watu ni kusaidia kupigana na uepukaji wa adhabu nchini kwa wanaofanya makosa.

Kulingana naye, hatua yake inachangiwa na mahakama kukosa kutendea Wakenya haki.

“Ninapigania haki ya Wakenya 40 milioni. Lazima turekebishe nchi hii na mahakama,” alisema.

Bw Sonko anakabiliwa na kesi kadhaa za ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka alipokuwa gavana wa Nairobi.

Alisema kuwa alianza kurekodi watu alipochaguliwa gavana katika juhudi za kurejesha imani ya umma katika ofisi ya gavana.

Hata hivyo, Bi Wanjira anapuuza kauli yake akihoji kuwa baadhi ya aliyorekodi hayahusiani na majukumu ya ugavana bali ni maisha ya kibinafsi ya watu.

You can share this post!

PAA sasa kuwika kote ikijitafutia umaarufu kisiasa

Usalama: Wakuu wahakikishia raia

T L