• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Supkem yashutumu serikali kwa mauaji

Supkem yashutumu serikali kwa mauaji

Na CECIL ODONGO

BARAZA la Kitaifa la Waislamu Nchini (SUPKEM) limekashifu utovu wa usalama unaoendelea kushuhudiwa nchini, likidai kuwa serikali inahusika na kupotea kwa baadhi ya watu katika njia ya kutatanisha.

Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado na mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Viongozi wa Waislamu (NAMLEF) Sheikh Abdullahi Abdi, jana walisema serikali haina tena nia ya kuhakikisha wanaotuhumiwa kushiriki uhalifu wanafikishwa korti, ila sasa inahakikisha wanapotea wasionekane tena na jamaa zao.

“Waislamu ndio wameathirika zaidi kutokana na vitendo vya watu kupotea katika njia ya kutatanisha, shughuli ambayo inadhaminiwa na maafisa wa usalama wa serikali. Inashangaza kuwa mauaji yanaendelea kukithiri na baadhi ya washukiwa wanapotea tu bila hata mkondo wa kisheria kufuatwa kuhusiana na madai dhidi yao,” akasema Ole Naado wakati wa kikao na wanahabari mtaani Hurlingham, Nairobi.

Bw Naado alisema kuwa serikali inadhihirisha mfano mbaya hasa kwa vijana wa Kiislamu na uongozi wa dini hiyo kwa kupuuzilia mbali sheria na kuendesha maangamizi dhidi ya raia bila kujali.

Polisi wamekuwa wakilaumiwa kwa kuhusika na mauaji mengi ambayo yamekuwa yakiripotiwa hapa nchini. Maafisa sita wa usalama wanakabiliwa na kesi kortini kutokana na mauaji ya ndugu wawili kule Kianjokoma, Kaunti ya Embu mapema mwezi huu.

Aidha, kumekuwa na visa vya watu kupotea kisha miili yao kupatikana maeneo tofauti hasa Ukanda wa Pwani huku mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yakidai polisi wanahusika.

“Kuendelea kudorora kwa usalama kunatia wasiwasi hasa miongoni mwa Wakenya wakati huu kampeni za kuelekea 2022 zimeanza kuchacha,” akaongeza.

Aidha, Sheikh Abdi alisifu idara ya mahakama kwa kutupilia mbali mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema hilo linaashiria uhuru wa idara hiyo.

“Tunawashukuru majaji wa mahakama kuu na ile ya rufaa. Majaji hao waliwapa Wakenya matumaini wakati ambapo tulikuwa tunakata tamaa hasa katika uhuru wa idara zetu za kikatiba,” akasema Sheikh Abdi.

Viongozi hao walitoa wito kwa maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake na wakataka viongozi wajikite katika kukamilisha miradi waliyoahidi wananchi mnamo 2017 kabla ya kura ya 2022.

You can share this post!

Chama kipya Pwani kinavyotishia Ruto na Raila

Ole Lenku aenda Uarabuni kuokoa msichana anayeteswa