• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Tunaomba uvumilivu kidogo tu tunatengeneza uchumi, Weta na Mudavadi wasihi Wakenya

Tunaomba uvumilivu kidogo tu tunatengeneza uchumi, Weta na Mudavadi wasihi Wakenya

Na SHABAN MAKOKHA

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa wamewataka Wakenya kusaidia Rais Ruto kupambana na changamoto zote katika juhudi zake za kuboresha Kenya.

Viongozi hao, walioongea Jumapili katika eneo bunge la Shinyalu, kaunti ya Kakamega, walisema serikali yake Rais Ruto inatafuta njia za kuongeza mapato kwa wananchi.

Miongoni mwa njia za kutoa afueni kwa Wakenya ni kufuta madeni katika sekta ya sukari, kupunguza bei ya pembejeo za kilimo, kuwapiga jeki wafanyabiashara wadogo kupitia mikopo ya Hazina ya Hasla.

Walisema hatua hizo zinalenga kuwawezesha kiuchumi wananchi wanaokabiliwa na kero la ongezeko la bei ya bidhaa za kimsingi na mafuta.

Bw Ichungwa alisema tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta linakumba dunia nzima na akawasuta viongozi wa upinzani kulimbikiza lawama kwa serikali.

“Hatutakubali kuhadaiwa na waongo ambao wanataka kutumia changamoto ya kiulimwengu ya kupanda kwa bei ya mafuta kutuangusha. Tutawasaidia wakulima wa miwa kwa kufuta madeni ya kampuni za sukari na kupunguza bei za pembejeo za kilimo. Wakati huu, tunawaomba wananchi wavumilie kwa muda mfupi tu baadaye tutafurahia,” akasema Bw Ichungwa.

Bw Mudavadi alishutumu viongozi wa upinzani kwa kile alichokitaja kama hatua ya wao kuhujumu utawala wa Rais Ruto ilhali “walichangia katika kuporomoka kwa uchumi wetu”.

Bw Mudavadi alishutumu chama cha ODM kwa kumhangaisha yeye na Bw Wetang’ula walipokuwa wakishirikiana kisiasa na kiongozi wake, Raila Odinga.

“Walimwondoa Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Seneti na wakapanga njama ya kumaliza Ford Kenya na ANC lakini wakafeli. Leo wanatoa madai kuwa Kenya Kwanza inawalenga. Ninawaomba wabadilishe mbinu zao za kisiasa ambazo zimepitwa na wakati,” akasema Bw Mudavadi.

  • Tags

You can share this post!

Kitabu kuelimisha sheria za mazingira na kuyahifadhi  

Kahawa yageuka kuwa chungu kwa Gachagua

T L