• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kahawa yageuka kuwa chungu kwa Gachagua

Kahawa yageuka kuwa chungu kwa Gachagua

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine amekiri kwamba serikali ya Kenya Kwanza inaonekana kulemewa na juhudi za kuleta mageuzi katika sekta ya kahawa nchini.

Hii ni licha ya Bw Gachagua na Rais William Ruto kutangaza “vita vikali” dhidi ya watu wenye ushawishi ambao wamekuwa wakidhibiti sekta hiyo kwa muda mrefu.

Akihutubu Jumapili katika eneobunge la Othaya, Kaunti ya Nyeri, wakati wa ibada ya maombi katika Kanisa la PCEA Kagere, Bw Gachagua alisema kuwa kinyume na sekta nyingine za kilimo, ambazo wameanza kuona matokeo ya mageuzi yanayoendelea, sekta ya kahawa imegeuka kuwa kizungumkuti kwa serikali.

“Tunafanya vizuri katika sekta ya maziwa kwani kwa sasa, lita moja ya maziwa inauzwa Sh50 kiwastani. Mwelekeo katika sekta hiyo ni mzuri. Pale tulipolemewa kabisa ni sekta ya kahawa. Hatujalemewa kwa sababu sisi ni wavivu au tumeshindwa kufanya kazi. Ni kwa sababu makateli yanayodhibiti sekta hiyo yana nguvu sana. Makateli hayo yamejipanga. Watu watatu au wanne ndio wamekuwa wakila jasho la wakulima. Huwa wananunua kahawa yetu kwa bei duni, na huwa hawatwambii ni kiasi kipi. Baadaye, huwa wanaenda na kuwauzia Wazungu kwa bei ghali, ambapo huwa wanakula faida wanayopata,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua anatoa kauli hiyo siku chache baada ya kurejea nchini kutoka Colombia, alikokuwa ziarani kwa siku kadhaa “kupigia debe kahawa ya Kenya ughaibuni”.

Kabla ya kusafiri nchini humo, Bw Gachagua alikuwa amesema kuwa lengo lake kuu lingekuwa kuwarai raia wa kigeni kususia kununua kahawa wanayouziwa na watu hao.

“Nikifika Colombia, nitawaambia watu kutoka mataifa mengine kutonunua kahawa kutoka kwa watu hao na badala yake kununua kutoka kwa wakulima kutoka Kenya, ili kuhakikisha wanawafaidi,” akasema Bw Gachagua kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, muda mfupi kabla ya kusafiri nchini humo.

Mnamo Januari, kwenye mahojiano mengine, Bw Gachagua alikuwa amewarai wakazi wa Mlima Kenya “kumwombea, kwani vita alivyokuwa akikabiliwa navyo kutoka kwa makateli hao ni vikubwa sana”.

“Nawarai mniombee. Hisi vi vita vya kawaida. Makateli hao wana nguvu sana. Niombeeni nipate nguvu ya kuyakabili,” akasema.

Kulingana na wadadisi, huenda kauli hiyo ikaisawiri vibaya serikali ya Kenya Kwanza, ikizingatiwa moja ya ahadi zake kuu ilizotoa kwa wenyeji wa Mlima Kenya ilikuwa ni kulainisha ufugaji, kilimo cha kahawa na majanichai.

Kwenye Agizo la Kwanza Kuhusu Mpangilio wa Serikali mnamo Januari, Rais Ruto alimpa Bw Gachagua jukumu la kuendesha mageuzi katika sekta ya ufugaji, kahawa na majanichai, ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kutokana na kilimo cha mazao hayo.

Mnamo Juni, Bw Gachagua aliongoza Kongamano Maalum la Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Kahawa mjini Meru, ambapo aliapa kufanya kila juhudi kuhakikisha amewaondoa mabroka wote ambao wamekuwa wakiwanunulia kahawa wakulima kwa bei duni.

Duru ziliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba baadhi ya wakulima katika ukanda wa Mlima Kenya wameanza kung’oa zao hilo, wakilalamikia bei duni licha ya ahadi ya serikali kuiboresha.

Katika baadhi ya maeneo, wakulima wameripotiwa kulipwa kati ya Sh32 na Sh40 kwa kilo moja ya zao hilo, ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo bei ya wastani ya zao hilo ilikuwa Sh100 kwa kilo moja.

  • Tags

You can share this post!

Tunaomba uvumilivu kidogo tu tunatengeneza uchumi, Weta na...

Wakenya kuhudumiwa matatizo ya afya wakiwa nyumbani, Ruto...

T L