• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:55 AM
Ubaguzi: Weusi wafaa wajilaumu wenyewe

Ubaguzi: Weusi wafaa wajilaumu wenyewe

UBAGUZI wa rangi una historia ndefu duniani. Ni hali ambayo imefanya mamia ya watu kujitolea sabili takribani katika maisha yao yote kukabili maovu hayo.

Miongoni mwao ni wanaharakati Martin Luther King, Malcom X, Mahatma Ghandhi, mwanamuziki Bob Marley, Marcus Garvey, Booker T Washington kati ya wengine wengi.

Msukumo wao wa kujitosa kwenye juhudi za kukashifu ubaguzi huo ni kuwa ulielekezwa sana kwa Waafrika ambao walitekwa nyara kama watumwa na kusafirishwa Amerika na sehemu nyingine duniani kuhudumu kama watumwa.Nchini Amerika, harakati za kukabili ubaguzi ndizo zimekuwa jukwaa la kuchaguliwa kwa marais wengi, baadhi yao wakiwemo Barack Obama na Joe Biden.

Alipochaguliwa mnamo 2008 kama rais wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika, Obama aliahidi kuanza juhudi kali kukabiliana na maovu hayo.Waamerika wengi walikuwa na imani kuwa utawala wa Rais Obama ungeweka mikakati ya kitaasisi na kisheria kuhakikisha dhuluma hizo za kijadi zimefikia mwisho.

Ingawa serikali ya kiongozi huyo haikufaulu sana kuweka msingi thabiti wa kupambana na maovu hayo, kuchaguliwa kwake kulikuwa ishara kuwa dunia ilikuwa tayari kwa mapambazuko mapya ya kisiasa yasiyozingatia ubaguzi wa rangi.

Kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka uliopita, ubaguzi ndio ulikuwa miongoni mwa masuala yaliyochangia sana aliyekuwa rais wa taifa hilo, Donald Trump, kushindwa na Biden.Wakati wa utawala wake kati ya 2016 na 2020, Trump alilaumiwa sana kwa kuendeleza ubaguzi, hasa dhidi ya Waafrika-Waamerika.

Upeo wa maovu hayo ulikuwa wakati Mwamerika Mweusi George Floyd alipouawa kikatili na polisi Mweupe Derek Chauvin mwaka uliopita.Maandamano yalizuka kote duniani yakikashifu mauaji hayo kama ishara kwamba Trump alikuwa ameshindwa kabisa kukabiliana na ubaguzi wa rangi.

Licha ya maandamano hayo, Trump alionekana kutotishika, badala yake akiwalaumu Weusi kwa “kutojitokeza kikamilifu kutetea haki zao.”Ghadhabu zilizoibuka ndizo zilimfanya kutochaguliwa tena kama rais kwa muhula wa pili.

Hata hivyo, maswali yanayoibuka ni: Licha ya juhudi na mikakati ambayo tumeona ikiendeshwa duniani kukabili maovu hayo; Je, Weusi (Waafrika) wamechukua hatua zipi kujikomboa? Huenda tunawalaumu Wazungu bila sababu maalum? Kuna uwezekano Waafrika wanajisaliti wenyewe?Sababu kuu ya maswali hayo ni ripoti kuhusu visa vya Waafrika kubaguana wao kwa wao katika nchi zao wenyewe.

Visa hivyo vimekuwa vikiripotiwa sana katika mikahawa mikubwa mikubwa, viwanja vya ndege na maeneo ya burudani ya hadhi.Hapa nchini, si mara moja Wakenya wameandika malalamishi yao kwenye mitandao wakieleza jinsi walivyobaguliwa kama “Weusi” katika mikahawa ya kitalii Pwani na maeneo mengine.

Katika simulizi hizo za kutamausha, Wakenya huwa ndio wahusika wakuu. Wao hupendelea kuwahudumia vizuri raia wa kigeni kuliko ndugu zao wenyewe!Chini ya mwelekeo kama huo, bila shaka huenda ikawa vigumu kwa juhudi zilizioanzishwa watu maarufu kama Martin Luther kupata mafanikio.

Lazima Waafrika wenyewe wajikomboe katika nafsi zao kwanza kwa juhudi hizo kufaulu. Ni sharti waungane kama ndugu wamoja!La sivyo, ubaguzi utaendelea kuwa saratani isiyo tiba hata kidogo kwa vizazi na vizazi vijavyo.

  • Tags

You can share this post!

Shule zakataa amri ya KNEC kuhusu mtihani

VROOOM! hatimaye,hatimaye